WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezipongeza taasisi za dini
likiwemo Kanisa Katoliki kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa
huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.
Amesema kuwa kitendo cha Kanisa Katoliki cha kuamua
kuipandisha hadhi Hospitali ya Tosamaganga na kuwa Hospitali ya Rufaa kwa ngazi
ya Mkoa ni cha kishujaa kwani kitaufaanya mkoa wa Iringa kuwa na hospitali
mbili za rufaa na hatimaye kupunguza adha kwa wakazi wa mkoa huo kusafiri
kwenda mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kufuata huduma za kibingwa.
Ametoa pongezi hizo jana mara baada ya kuzindua hospitali ya
rufaa ya Tosamaganga ngazi ya Mkoa pamoja na huduma za mionzi kwenye hospitali
hiyo, iliyopo wilayani Iringa, mkoani Iringa.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Iringa kwa ziara ya kikazi ya
siku nne, amesema kuwa uamuzi wa kuipandisha hadhi hospitali hiyo ni kuunga
mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi
wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo yao.
“Dhamira ya Rais Dkt. Samia ni kuwatumikia wananchi kwa
kuhakikisha sekta ya afya inafika kila mahali ikiwemo kujenga hospitali kwenye
kila Halmashauri. Watanzania endeleeni kuwa na imani Serikali yenu, nasi
tutaendelea kuwahudumia ipasavyo.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt.
Benjamin Mfaume ameishukuru Serikali kwa misaada ya hali na mali inayotolewa
kwenye hospitali hiyo ili kuiwezesha kutoa huduma bora kwa Watanzania.
“Katika mwaka 2022/2023, Serikali ilitoa shilingi bilioni
2.2 zikiwa ni mishahara ya wafanyakazi, dawa kupitia MSD na Basket Fund kupitia
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na "OC" kupitia Serikali Kuu na hadi
sasa Serikali bado inaendelea kufanya hivyo,” alisema.
Alisema hospitali hiyo, inahudumia wagonjwa kati ya 62,000 hadi 78,000 kwa mwaka ikiwa ni wastani wa wagonjwa 7,000 hadi 8,000 kwa mwezi huku idadi kubwa ikiwa ni ya akinamama wajawazito na watoto.
0 Maoni