WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelipongeza Kanisa la Tanzania
Assemblies of God (TAG) kwa mkakati wake wa kukuza watoto kiimani huku
wakilijua na kulishika neno la Mungu.
“Pamoja na shughuli ya uinjilishaji, leo nimeshuhudia watoto
wadogo wakisema maneno ya Mungu bila kusoma mahali popote na mwingine
akiielezea Misingi ya Kanisa la TAG bila kusoma popote. Hii ni kazi kubwa,
mnasathili pongezi.”
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 14, 2024) wakati
akizungumza na viongozi na waumini wa Kanisa la TAG ambako alimwakilisha Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Miaka 85 yaliyofanyika kwenye
uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Amesema kanisa hilo linawafanya watu kuwa wamoja, kuwa na
uhusiano wa kiimani na kijamii na kutoa mafundisho ya umuhimu wa kushiriki
katika huduma kutoa misaada, elimu, huduma za afya na maendeleo ya jamii.
“Kanisa hili ni mfano katika kukuza umoja na ushirikiano
kati ya Wakristo wa madhehebu mbalimbali na waamini wa dini nyingine nchini,
kitendo ambacho kinatuwezesha kama jamii kuwa na mshikamano na kuimarisha amani
na usalama.
Waziri Mkuu amesema Serikali ina kila sababu ya kuwashukuru
Wachungaji na Maaskofu kwa kazi yao kubwa ambayo inaimarisha amani, utulivu na
maendeleo katika nchi.
“Serikali inathamini mchango wa taasisi za dini katika
kuimarisha maadili mema, kukemea maovu na mmomonyoko wa maadili. Wakati wote
Serikali imekuwa ikifanya kazi kwa pamoja na taasisi za dini hususani katika
kampeni za kijamii za kuelimisha na kuhamasisha maadili mema na mwenendo mwema
kwa wanajamii.”
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG Tanzania, Dkt.
Barnabas Mtokambali amewataka waumini wa TAG hilo wawe na maono makubwa ya
kuweza kulivusha kanisa hilo kwa miaka mingine 85 huku akiweka msisitizo kwa
vijana kuyabeba maono hayo.
“Wana TAG ninawasihi tuwe na maono makubwa, tufikiri na
kufanya mambo makubwa kwa miaka mingine 85 ijayo. Tuwe na umoja, upendo na
mshikamano na tuendelee kujituma na kujidhabihu kwa hali na mali ili mambo
makubwa yaweze kutokea,” amesisitiza.
Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa anayoifanya Bara na visiwani ya kuiletea nchi maendeleo na hasa kuboresha miundombinu.
Amesema kuanzishwa kwa safari za treni ya mwendokasi kutoka
Dar es Saalam hadi Morogoro ni hatua kubwa kwa Serikali katika kurahisisha
huduma za usafiri pamoja kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Binafsi, ninapoongelea maendeleo, naguswa na hii sekta ya
usafiri kwa sababu kwa miaka zaidi ya 10, nimekuwa nikisafiri kati ya saa nne
hadi tano kuja Dar es Salaam yalipokuwa Makao Makuu ya TAG. Na sasa sasa hivi
ofisi zimehamia Dodoma, nimekuwa nikienda huko. Itakapoanza safari za
mwendokasi mwezi huu kwenda Dodoma, nitakuwa nimeokoa muda wa saa sita, tatu
kwenda Dar es Salaam na tatu kwenda Dodoma,” alisema.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kudumisha amani, umoja, utulivu na uhuru wa kuabudu nchini. “Kutokana na kudumisha haya, imekuwa ni tunu ya kipekee ambayo imeliwezesha kanisa la TAG na madhehebu mengine nchini kupiga hatua kubwa sana za maendeleo.”
Mapema, Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Mchg. Joseph Marwa
alisema mbali na majukumu ya kutangaza injili, Kanisa hilo linatoa huduma za
kijamii pamoja na kukukuza maadili mema miongoni mwa waumini wake.
“Idadi ya wachungaji imeongezeka, makanisa yameongezeka na
kufikia 5,918; wainjilisti wamefikia 2,008; majimbo kwa sasa yako 71 na wilaya
ziko 860 kutoka 557 za awali, sawa na wilaya mpya 303.”
Alisema TAG inatoa huduma za jamii kwa kujenga shule za
msingi, sekondari, ina vyuo viwili vya ualimu, vituo vya watoto yatima 21,
vituo vya kulea watoto 89 na vyuo vya ufundi vitano ambapo kwa sasa chuo kipya
kinajengwa Manyara. “Kwa nchi nzima, tumeshachimba visima 293 ikilinganishwa na
153 vilivyo kuwepo zamani,” amesema.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Rais Mstaafu wa Benin, Thomas Boni Yayi, Wabunge, wamishenari, viongozi wa makanisa kutoka nchi 13 za Afrika na Asia, viongozi 60 kutoka makanisa ya Kipentekoste, wazee wa imani 10, waangalizi, wachungaji kutoka mikoa mbalimbali na washirika wa TAG.
0 Maoni