WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameishukuru Serikali ya Denmark
kwa misaada ambayo imekuwa ikiitoa kwenye miradi ya maendeleo nchini ambapo
Krona milioni 1.95 (sh. bilioni 645.86) zilizotolewa katika kipindi cha miaka
mitano.
Ametoa shukrani hizo leo (Jumatatu, Julai 15, 2024) wakati
akizungumza na Balozi wa Denmark anayemaliza muda wake nchini, Bi. Mette N.
Dissing-Spandet kwenye ofisi ndogo ya Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Serikali hiyo ilisaidia sana kwenye
miradi mbalimbali hasa katika sekta za afya, masuala ya kikodi, shughuli za
utafiti, hifadhi ya mazingira na kuimarisha demokrasia na utawala bora.
“Ninakushukuru kwa jitihada zako katika kipindi chote cha
miaka mitano uliyokuwepo hapa nchini kwani umesaidia kuimarisha mahusiano
yaliyokuwepo baina ya nchi hizi mbili tangu miaka ya 60. Pia tumenufaika na
programu za kubadilishana wataalamu baina ya nchi zetu,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema kutokana na changamoto za kiuchumi zilizokuwepo
duniani, mwaka 2020 nchi hiyo ilitaka kupunguza idadi ya balozi zake barani
Afrika, Tanzania ikiwemo. “Lakini Serikali yetu ilimtumia Balozi huyu kuelezea
haja ya kuendelea na mahusiano baina ya nchi zetu mbili na ikafanikiwa, ndiyo
maana tunatarajia kumpokea balozi mwingine hivi karibuni.”
Waziri Mkuu amesema anatarajia kuwa Balozi ajaye ataendeleza
mazuri ya mtangulizi wake ikiwemo kukamilisha mpango wa kuandaa kongamano la
wafanyabiashara baina ya Tanzania na Denmark ili kuwaalika wawekezaji kwenye
sekta za nishati, kilimo biashara na viwanda.
Amemuomba Balozi huyo akisharejea kwao, aendelee kuwa Balozi
mzuri wa kuitangaza Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ambayo ameyaona hapa
nchini.
Kwa upande wake, Balozi Dissing-Spandet alimweleza Waziri
Mkuu anaondoka nchini akiwa anaacha mahusiano baina ya nchi hizo mbili yakiwa
kwenye mikono salama kwa sababu Balozi anayekuja kuchukua nafasi yake ni
mwanadiplomasia mzoefu.
“Ninaondoka nchini nikiwa na furaha kwa sababu mahusiano ya
Tanzania na Denmark yamerudi kwenye hali yake ya awali. Ninashukuru kwa kipindi
chote cha miaka mitano nilichoishi hapa nchini, mbali na changamoto za UVIKO-19
na za kiuchumi duniani, kilikuwa ni kizuri sana na hakitasahaulika maishani
mwangu,” alisema Balozi huyo.
Amesema anaamini kuwa Balozi mpya ajaye atasimamia suala la uwekezaji ikizingatiwa kwamba nchi hiyo inaandaa mkakati mpya wa kuboresha mahusiano baina yake na nchi za Kiafrika, hasa kwenye eneo la uwekezaji.
0 Maoni