Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imetekeleza kwa
vitendo maagizo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu ya
kuchagua na kuendesha mafunzo ya vinara wa ufuatiliaji na uthamini katika
taasisi za umma.
Mmoja wa Waratibu wa mafunzo ya vinara yaliyotolewa na
wawezeshaji kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, hivi karibuni Bw. Elirehema Saiteru,
Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa TANROADS amesema kuwa wameendesha
mafunzo kwa watumishi kutoka Makao Makuu na mikoa yote 26 ya Tanzania, yaliyofanyika
mkoani Morogoro, kulingana na mwongozo uliotolewa mwezi Juni 2024 jijini
Dodoma.
Bw. Saiteru amesema kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa
mwongozo wa kuchaguliwa kwa vinara watakaokuwa wakifanya ufuatiliaji na
tathimini ya miradi iliyopo chini ya taasisi hii.
“Baada ya uzinduzi wa hii miongozo kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu tulipewa maelekezo kuanza mara moja utekelezaji wake, na awali kama
taasisi tulikuwa tayari tumeshaanza kuandaa miongozo yetu na sasa tupo katika
nafasi nzuri ya utekelezaji kwa kuwa inakwenda sambamba,” amesema Bw. Saiteru,
Hatahivyo, amesema hatua inayofuata ni kuandaa nyaraka ya
upimaji utayari wa taasisi wa kufanya kazi ya ufuatiliaji na tathmini.
Mwakilishi wa washiriki, Mhandisi Cecilia Kalangi ameshukuru
kwa taasisi kuendesha mafunzo haya, ambayo yatasaidia kupata ufumbuzi wa haraka
kwenye miradi yenye changamoto tangu awali.
Nawe Mha. Magesa Chacha, Mkuu wa Idara ya Mipango kutoka
TANROADS mkoa wa Mwanza amesema washiriki wameweza kujifunza namna ya kufanya
ufuatilia na tathmini kwa kuzingatia maono ya Dunia na ya serikali ya mwaka
2025 na pia mifumo iliyoibuliwa na Wizara ya Ujenzi ya kuweka taarifa zote za
miradi.
“Nawasihi washiriki wenzangu kuzingatia kila hatua ya
mafunzo haya kwani ndio mwarubaini ya miradi ambayo baada ya kuanza inaonekana
ikiwa na changamoto, wakati ingeweza kutambulika katika hatua za awali
ingetatuliwa mapema,” amesisitiza Mha. Kalangi.
Naye mwezeshaji Bw. Chalton Meena kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu amesema ofisi hiyo inasimamia utendaji wa serikali
kwenye wizara na taasisi zake, hivyo wote hawana budi kufuata mwongozo huo wa
mwaka 2024.
Bw. Meena amezitaja nyaraka hizo kuwa ni Mwongozo wa Tathmini wa Kitaifa (National Evaluation Manual); Mwongozo wa Usimamizi wa Tathmini nchini na Ufuatiliaji na Tathimini (Monitoring & Evaluation Readness Assessment Tool for Government Institutions).
0 Maoni