Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) ametembelea
Hifadhi ya Taifa Gombe inayosifika kwa utalii wa Sokwe Mtu barani Afrika na
kuahidi kuifungua barabara ya kutoka Mwandiga kwenda Kagunga hadi mpakani mwa
Burundi ili kuvutia watalii wengi kutembelea hifadhi hiyo.
Akiwa ndani ya hifadhi hiyo, Bashungwa alisema, “Serikali
inafanya jitihada za dhati na haraka kuhakikisha barabara ya kutoka Mwandiga
kwenda mpakani Kagunga kupitia Mwamgongo inafunguliwa ili watalii wanaotokea
Burundi waje pia katika hifadhi zetu za Gombe na Mahale.”
Aidha, Bashungwa aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya
Ujenzi itaendelea kushirikiana na TANAPA kusaidia barabara zinazoelekea ndani
ya hifadhi zote zilizoko mkoani Kigoma ili kupunguza adha kwa watalii wa ndani
na nje wanaotembelea hifadhi hizo.
Awali akimkaribisha katika hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi
wa Uhifadhi, Yustin Njamas ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Gombe alisema,
“Barabara ya Mwandiga hadi Kagunga itakapokamilika tunatarajia kupata watalii
wengi kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuongeza pato la
Taifa na kuchangia uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa wakazi wa mkoa wetu wa
Kigoma.”
Hata hivyo, Kamishna Njamas alimueleza Waziri Bashungwa kuwa
licha ya hifadhi hiyo kusifika kwa utalii wa Sokwe Mtu, pia hifadhi hiyo ina
mazao mengine ya utalii kama vile utalii wa kuvua samaki, utalii wa kupiga
kasia na utalii wa kutembea kwa miguu kuangalia nyika na bahari zilizosheheni
utitiri wa baioanuai za nchi kavu na majini.
Waziri Bashungwa ametembelea hifadhi hiyo Julai 11, 2024 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philipo Mpango wakati wa ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo mkoani Kigoma.
0 Maoni