Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),
imekamilisha ujenzi wa daraja la Berega lililopo katika barabara ya Berega - Dumbalume
lenye urefu wa mita 140 na upana mita 11 katika Halmashauri ya Wilaya ya
Kilosa, mkoani Morogoro.
Kukamilika kwa daraja hilo limeweza kuunganisha Wilaya ya
Kilosa, Gairo, Kiteto na Kilindi na hivyo kuondoa kero ya miaka mingi iliyokuwa
ikiwakabili wananchi katika shughuli za usafiri na usafirishaji ikiwemo
kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Kaimu Meneja wa TARURA
Wilaya ya Kilosa Mhandisi Winston Munyanga alisema ujenzi wa daraja la Berega
umekamilika kwa asilimia 100 pamoja na maboresho ya barabara ya Berega –
Dumbalume yenye urefu wa Km 7 ambayo yamegharimu shilingi Bilioni 7 na kuondoa
kero ambayo wananchi wa Wilaya hiyo na
zile za jirani walikuwa wanazipata.
”Kwa sasa ujenzi wa daraja la Berega umekamilika na
tumefanikiwa kuunganisha Wilaya ya Kiteto, Gairo, Kilosa na Kilindi pamoja na
kurahisisha huduma za kijamii na kiuchumi kwa kuzifikia kwa urahisi hasa shule pamoja na hospitali
zilizopo ng’ambo ya daraja hilo,” alisema Mhandisi Winston.
Pia, Mhandisi Winston ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ongozeko la bajeti kwa Wakala
wilayani Kilosa ambayo imewezesha kutekeleza mradi huo mkubwa wa ujenzi wa
daraja la Berega ambalo limekamilika na kuwawezesha wananchi kutumia daraja
hilo katika kipindi chote cha mwaka, pamoja na kusafirisha mazao yao na
kufikisha sokoni kwa wakati.
Naye, Diwani wa Kata ya Berega, Mhe. Filemoni Maube alisema
wanaishukuru Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa daraja la Berega kwani hapo
awali kipindi cha masika wananchi wa Kata hiyo walikuwa wanapata tabu katika
shughuli zao za kijamii na kiuchumi na iliwalazimu kusubiri maji yapungue ndipo
waanze kupita.
”Tunaishukuru sana Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa daraja
ili kwa sababu sasa tuna uhakika wa kupita hapa katika vipindi vyote tofauti na
hapo awali, wanafunzi wataweza kufika shuleni, wagonjwa watafika hosptalini
pamoja na kusafirisha mazao yetu kwa urahisi”, alisema Mhe. Filemoni
Aidha, Bw. Gideon Mshala, Mkazi wa Kijiji cha Berega
ameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha ujenzi wa daraja hilo
ambalo limewasaidia wananchi wa Kata ya Berega, Kiegeya na maeneo jirani kuvuka
kwa urahisi na kuzifikia huduma za kijamii tofauti na hapo awali ambapo daraja
lilikuwa limekatika.
”Tunaishukuru sana Serikali kwa kukamilisha daraja hili,
tulikuwa tunapata tabu katika kuzifikia huduma za kijamii pamoja na kusafirisha
mazao yetu kama mbaazi, miwa, mahindi na viazi kwa kuwa wakazi wengi wa huku ni
wakulima hivyo tulivyokosa huduma ya daraja tulipata tabu katika shughuli zetu
za usafiri na usafirishaji,” alisema Gideon.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA unaendelea kutekeleza miradi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wananchi wanafika kusiko fikika.
0 Maoni