Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Nchini - TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko amewahimiza
watanzania kuchangamkia fursa za ufugaji wa wanyamapori zinazopatikana katika
Taasisi ya TAWA.
Ameyasema hayo jana alipotembelea banda la Wizara ya
Maliasili na Utalii Katika Maonesho ya 48 ya biashara ya Kimataifa ambayo kwa
Mwaka 2024 leo yamefikia tamati.
"Sehemu kama Afrika ya Kusini ufugaji wa wanyamapori ni
mkubwa sana, kwahiyo mimi natoa rai kwa wananchi hasa watanzania kuingia katika
biashara hiyo ya ufugaji wa wanyamapori" amesema.
Aidha, Meja Jenarali (Mstaafu) Semfuko amesema ili
watanzania waweze kupata kitoweo cha nyamapori kwa urahisi wanapaswa kuingia
katika biashara ya ufugaji wa wanyamapori na kwakufanya hivyo wataziwezesha
bucha za wanyamapori kufanya kazi vizuri.
Sambamba na hilo, Semfuko amesema TAWA ina mipango mingi ya
kuhakikisha inapata wawekezaji wakubwa
na wadogo ili wawekeze katika maeneo mbalimbali inayoyasimamia kama vile
kuwekeza katika mahoteli, vitalu vya uwindaji wa kitalii na ranchi za
wanyamapori ili kuongeza idadi ya wanyama hao.
Maonesho ya 48 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yenye kauli mbiu "Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji" yalianza Juni 28, 2024 na kuzinduliwa rasmi Julai 03, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Nyusi ambapo leo Julai 13, 2024 yamefungwa na Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Na. Beatus Maganja- Dar es Salaam



0 Maoni