Tamasha la Utamaduni wa Watu wa Kigoma lahitaji milioni 378

 

Shilingi za Kitanzania 378,000,000 zinahitajika kufanikisha Tamasha la Utamaduni wa watu wa Kigoma ambalo linatarajiwa kufanyika katika kijiji cha makumbusho Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi Agosti, 2024.

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) wakati wa uzinduzi wa harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya kufanikisha tamasha la utamaduni wa watu wa Kigoma katika ukumbi wa Kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es Salaam.Mhe. Kitandula alisema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inatambua mchango mkubwa unaotolewa na tamaduni mbalimbali za kitanzania katika kukuza zao la utalii wa kiutamaduni.

“Utamaduni una umuhimu mkubwa sana hasa katika kudumisha umoja na  utambulisho wa Taifa na  ukitumiwa vyema ni zao muhimu sana katika  kukuza Utalii na hivyo kuwainua wananchi kiuchumi,” alisema Mhe. Kitandula.

Mhe Kitandula ambaye alimuwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika harambee hiyo aliongeza kwa kumnukuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye aliwahi kusema “Taifa Lisilo na Utamaduni wake ni Taifa Mfu” ndiyo maana Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutambua hili inajivunia kuwa na wanajamii wanaothamini utamaduni wao na itaendelea kuwaunga mkono.

Akimkaribisha Mhe. Kitandula Mjumbe wa Bodi ya Makumbusho ya Taifa Dkt. Mboni Ruzegea ambaye alimuwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Makumbusho alisema kuwa siku ya utamaduni wa Mtanzania ni tamasha lililobuniwa na bodi ya makumbusho ya Taifa mwaka 1994 ili kutoa fursa kwa jamii mbalimbali hapa Nchini kuonesha tamaduni zao katika kijiji cha makumbusho.

Dkt Mboni aliongeza kuwa Tamasha tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994, zaidi ya jamii 36 zimeonyesha mila na desturi zao kwa watanzania na wageni mbalimbali. Tamasha hili huonyesha nyumba za asili za jamii husika, vyakula na vinywaji vya asili, vifaa vya jadi vinanyoonyesha maisha halisi ya jamii, masuala ya maendeleo na fursa za uwekezaji kwenye mikoa na wilaya.

Aidha, katika harambee hiyo ya kwanza kiasi cha shilingi 81,533,199 ziliahidiwa kwa ajili ya kufanikisha Tamasha la siku ya utamaduni wa Mtanzania 2024.

Na Anangisye Mwateba-Dar es Salaam

Chapisha Maoni

0 Maoni