WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameendesha harambee na
kuchangisha sh. milioni 928.67 za ujenzi wa kanisa kuu tarajiwa la Mt. Andrea
Kagwa la Jimbo Katoliki la Lindi.
Kati ya fedha hizo, sh. milioni 464.3 ni fedha taslimu na
nyingine kati ya hizo zimeshawekwa benki na sh. milioni 464.37 bado ni ahadi.
Awamu ya kwanza ya ujenzi huo, inatarajiwa kugharimu sh. milioni 700.
Akizungumza na waumini na wadau mbalimbali waliohudhuria
harambee iliyofanyika Ruangwa mjini, leo mchana (Jumamosi, Julai 27, 2024),
Waziri Mkuu amewataka waliotoa ahadi wazikamilishe mapema ili kazi ya ujenzi
isikwame.
"Ninawashukuru sana wote mliofika na wote waliochangia
ujenzi wa kanisa tarajiwa. Ninawaomba walioahidi, wakamilishe ahadi zao mapema
ili kazi ianze kwani ramani ipo, mafundi wapo tayari, wasimamizi wa ujenzi wapo," amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema uamuzi wa Baba Askofu wa Jimbo Katoliki
la Lindi, Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa kuanza ujenzi wa kanisa kuu la jimbo
hilo, ni utekelezaji wa maono aliyokuwa tangu aliposimikwa kuongoza jimbo hilo
Juni, 2022.
"Mhashamu Baba Askofu Pisa ameanza kutekeleza maono
yake kupitia kaulimbiu ya NINAONA KIU aliyoitangaza tarehe 26 Juni, 2022 wakati
akisimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi. Ninawaomba wanaLindi tumpe
ushirikiano kwa sababu maono yake ni endelevu. Ninawasihi tumpe ushirikiano ili
aweze kutimiza hayo maono."
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wazazi na walezi
wawe karibu na watoto wao na wafuatilie hatua za ukuaji wao ili baadaye wawe
raia wema.
Mapema, akisoma risala kuhusu mradi wa ujenzi wa kanisa
tarajiwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Mhandisi Fortunatus Machibya alisema
harambee hiyo imelenga kukusanya sh. milioni 900 ambapo kati ya hizo, sh.
milioni 700 ni za ujenzi na sh. milioni 200 ni za maandalizi ya Jubilei ya
miaka 25 ya upadrisho wa Askofu Pisa na miaka 50 ya Askofu Mstaafu wa Jimbo la
Lindi, Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani.
Alisema ujenzi wa kanisa hilo unahitajika kukamilika haraka
kwa sababu wakati Jimbo Katoliki la Lindi linaanzishwa mwaka 1986, kanisa
lililopo lilipewa tu hadhi na hapakuwa na kanisa jipya.
"Kanisa lililopo ni dogo, ni la zamani na uwezo wake ni kuchukua watu
600 wakati matukio ya kikanisa huwa yanaleta watu zaidi ya 1,000. Tumeamua
kujenga kanisa jipya badala ya kufanya ukarabati na kupoteza fedha. Hili
tutalijenga kwa awamu kwa miaka mitano, na hadi likamilike, tunatarajia kutumia
shilingi bilioni 6.6," alisema.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Mhashamu Titus Mdoe, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Tellack na viongozi mbalimbacli wa mkoa huo.
0 Maoni