RC Batilda atabiri makubwa Dira ya Taifa 2050

 

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amesema utekelezaji wa agizo la Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kuhusu ushirikishaji umma, unatoa fursa pana kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuwa bora zaidi na yenye tija kwa nchi na watu wake.

Mhe Balozi Dk Batilda, ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha, kwenye Kongamano la Pili la Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, lililofanyika leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Kongamano hilo la siku moja lilifunguliwa na kufungwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Amesema, ushirikishaji wa makundi mbalimbali ya kijamii kutoka sekta za umma na binafsi, kunafungua uwanda mpana zaidi wa kupata maudhui yanayobeba mahitaji na maono halisi ya Watanzania ifikapo 2050.

Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe Stanslaus Nyongo, amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuonesha mahali na namna ambayo Watanzania wanataka kufikia katika kipindi cha kati ya 2025 hadi 2050.

Kwa upande wake, Dk Asha-Rose Migiro, akasema maoni ya wananchi kupitia kongamano hilo, yanachukuliwa kwa umakini na ‘kuzibeba’ hoja zenye maslahi ya kuanzia ngazi za chini kwenye jamii.

Dk Migiro amesema baada ya kukamilisha kwa mchakato wa kukusanya maoni hayo, yatarejeshwa kwa wananchi kabla ya kuchapwa na kuwasilishwa kwenye vyombo vya uwakilishi kwa hatua zaidi.

Na Mashaka Mgeta- Arusha

Chapisha Maoni

0 Maoni