Kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 ni halali
na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi kuu zijazo bila kujali mabadiliko ya
jina la Tume ya Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi.
Akizungumza wakati wa ziara aliyoifanya ya kukagua vituo vya
kuandikishia wapiga kura leo tarehe 22 Julai, 2024 katika Halmashuari ya Wilaya
ya Kasulu, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw.
Kailima Ramadhan amesema wapiga kura wenye kadi hizo hawahusiki na zoezi la
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Naomba nitoe wito kwa wale ambao kadi zao ni zile zenye
jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wanadhania kuwa kubadilika kwa jina la
Tume kunasababisha kubadili kadi watambue kuwa kadi zao ni halali kwa mujibu wa
kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya
Mwaka 2024,” amesema.
Mkurugenzi huyo wa uchaguzi ambaye kwenye ziara yake
aliambatana na Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kasulu Vijini, Bw. Emmanuel
Ladislaus na maafisa wengine waandamizi, alieleza kwamba wenye kadi hizo ambazo
zimeharibika, zimepotea au wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo
lingine wanahusika kwenye zoezi hilo.
“Nimebaini kuwa wapo wapiga kura wenye kadi za zamani zilizotolewa kabla ya mwaka 2015
(zile za karatasi) hao waje vituoni ili waandikishwe upya kwa kuwa mfumo
uliotumika wakati huo ni tofauti na mfumo wa sasa,” amesema.
Bw. Kailima
amewakumbusha wananchi wa mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi kuwa zimebaki siku
tatu kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kukamilika
kwenye mikoa yao, hivyo, ni muhimu kujitokeza kwa wingi na kutumia vizuri siku
hizo.
Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo umeanza tarehe 20
Julai, 2024 na utafanyika kwa siku saba hadi tarehe 26 Julai, 2024 ambapo vituo
vinafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
0 Maoni