Dada wakazi aliyemchinja mtoto wa bosi wake akamatwa

 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kumkamata dada wa kazi aliyefahamika kwa jina la Clemensia Mirembe (19) aliyekuwa anatafutwa kwa kutenda kosa la kumchinja shingo mtoto wa bosi wake.

Tukio hilo lilitokea Julai 17, 2024 ambapo dada huyo wa kazi alimjeruhi kwa kitu chenye ncha kali maeneo ya shingoni mtoto Malick Hashim (6) anayeishi eneo la Goba Kinzudi, Kinondoni ambapo baada ya tukio mtuhumiwa alikimbia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 22, 2024 na Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema upelelezi wa tukio hilo la kikatili ulianza mara moja na jana Julai 21, 2024 saa 4:00 usiku Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.

Kamanda Muliro amesema mtuhumiwa huyo anahojiwa kwa kina na atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kwa hatua zaidi za kisheria.

Mtoto huyo amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na tayari wamemfanyia upasuaji mkubwa ambao ulichukua muda wa saa nne ili kurekebisha njia ya hewa, sanduku la sauti, matezi yaliyopata changamoto kwenye shingo na kutibu jereha la nyuma ya shingo.

Tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema atalipia gharama zote za matibabu za mtoto huyo.

Chapisha Maoni

0 Maoni