Simba kuwafuata Simba wa Mikumi uzinduzi Simba Day

 

Timu ya Simba SC imepanga kwenda mkoani Morogoro kwa kutumia usafiri wa treni ya kisasa kwa  kutumia reli SGR kufanya uzinduzi wa kuelekea Simba Day kwenye Hifadhi ya Mikumi, lengo likiwa ni kutangaza utalii na kukutana na mnyama simba pamoja na kutangaza uasafiri wa treni ya SGR.

Mtendaji Mkuu wa Simba Imani Kajula amesema wanakwenda kuzindua Simba Week ndani ya mkoa wa Morogoro ndani ya Hifadhi ya Mikumi, kwa kuwa Simba ni timu ya watu wote ndio maana wamewapa heshima Wanasimba wa Morogoro kufanya uzinduzi na kitovu itakuwa Mikumi.

"Kwenye mbuga ya Mikumi sio tu kufanya uzinduzi na kurudi, kuna uwanja mzuri sana wa mpura na Ahmed atazungusha namba 6, yawezekana pia Ally Kiba akawepo. Mimi nitazungusha namba 10,  Ubaya Ubwela hadi kwenye mbuga za wanyama,"  alisema Kajula.

"Wiki ya Simba itakuwa na mambo mengi kama kusaidia jamii, kuamsha hamasa ya mashabiki, kuenzi waasisi wa Simba lakini pia michezo ni sehemu ya utalii ndio maana mara nyingi sana Simba tumekuwa tukioanisha mikakati yetu na ya utalii," alisema Kajula.

"Hatutaenda Mikumi moja kwa moja, tutaanzia Morogoro mjini. Tutaenda na kurudi na hilo linawezekana sababu ya usafiri wa haraka wa SGR. Klabu ya Simba tunatambua jukumu letu kusaidia kutangaza vivutio vyetu,” alisema Kajula.

Amesema Tanzania ni nchi ya tatu kwa vivutio duniani hivyo Simba kama klabu inajali wajibu wake kwa serikali. “Na lingine niwambie Mikumi ndio mbuga inayoongoza kupokea watalii wengi wa ndani."

Kwa upande wake Msemaji wa Simba Ahmed Ally alisema watafanya utalii mbugani na baada ya hapo watacheza mechi na kisha kurudi Morogoro mjini na kuanza sfaari kurudi Dar es Salaam. “Safari yetu itakuwa tarehe 24, Julai 2024. Tutakwenda na kurudi lakini kama ukitaka kulala Morogoro unaruhusiwa."

"Safari yetu itakuwa ni Julai 24, 2024 na treni itaondoka Dar es Salaam saa 12:00 alfajiri, muda wa kufika kituoni ni saa 11:00 alfajiri. Wale wote ambao wanatamani kuungana nasi kuelekea Morogoro kufika kwa wakati. Tutafika Morogoro saa 1:30 asubuhi,” alisema Ally.

Amesema hadi sasa wamekodi behewa tatu kwa ajili ya Wanasimba na kwa mashabiki wao na kuongeza kuwa hakutakuwa na nauli. “Kila shabiki wa Simba ambaye anahitaji kuandika historia kupanda SGR, kufika Mikumi, kushiriki uzinduzi wa Wiki ya Simba afike akiwa na jezi ya Simba."

"Tukifika Morogoro tutakuta Wanasimba wenzetu wamekuja kutupokea. Kwa hili niyashukuru matawi ya Simba Morogoro. Tunataka kwenda kuishangaza Morogoro na ninyi mnatujua sisi sio watu wa kufanya mambo madogo madogo, tunafanya kwa ukubwa wake,” alisema Ally.

Naye Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania, Nassor Garamatatu alisema wameingia ushirikiano huu kwa sababu kuu mbili, moja kuhamasisha utalii wa ndani na nje kupitia uzinduzi wa Wiki ya Simba.

Ametaja sababu nyingine kuwa wanafahamu ushawishi klabu ya Simba imekuwa nao kwenye mitandao ya kijamii. “Wamefanya kampeni nyingi za aina hii kama ya mwaka jana kwenda Mlima Kilimanjaro na Visit Zanzibar hivyo tunaamini kampeni hii itatoa hamasa kwa Watanzania kwenda kwenye vivutio vilivyo karibu nao kwa kutumia treni ya SGR."

"Simba inakuja Mikumi na Mikumi kuna Simba. Mnakuja kukutana na Simba wa kweli. Tunawakaribisha sana na tunawashukuru sana kwa kutupa heshima ya kuja kuzindulia Simba Week kwenye hifadhi yetu," alisema Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi, Agustino Masesa.

Chapisha Maoni

0 Maoni