Hifadhi ya Msitu Asili Matogoro yenye mandhari ya kuvutia ni
kichocheo adhimu na muhimu cha kukuza utalii katika mikoa ya kusini hususan
mkoa wa Ruvuma kutokana na kubeba hazina kubwa ya kihistoria ikiwemo uwepo wa
mapango makubwa yaliyotumika wakati wa vita ya majimaji.
Haya yamebainishwa na Naibu waziri wa maliasili na Utalii,
Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipofanya ziara ya kujionea fursa za kiutalii
zinazopatikana katika Hifadhi ya Msitu Asilia Matogoro iliyopo Wilayani Songea
Mkoa wa Ruvuma.
Aidha, hifadhi hii ya Msitu Asilia na milima yake imebeba
jukumu kubwa la uhai na ustawi wa watanzania kutokana na ukweli kuwa Hifadhi
hii ni chanzo cha mito mitatu mikubwa na muhimu ambayo ni Ruvuma unaomwaga maji
yake kwenye bahari ya Hindi, Luwegu ambao unachangia asilimia 19 ya maji kwenye
mto Rufiji na kisha kuingia bahari ya Hindi, na Mto Luhira ambao ni chanzo cha
mto Ruhuhu ambao unamwaga maji yake kwenye Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Kitandula alitoa wito kwa wawekezaji wanaotaka
kuja kuwekeza katika eneo hilo lenye mandhari nzuri na ya kuvutia ambayo inafaa
kwa utalii wa kupanda milima, utalii wa picha, utalii wa kuruka kwa puto na
utalii wa ikolojia kukimbilia na kuikumbatia fursa hiyo.
Vilevile Mhe. Kitandula ameutaka uongozi wa Wakala wa Huduma
za Misitu Tanzania (TFS) ambao unasimamia eneo hilo kulitangaza kwa
kuliunganisha na matamasha mbalimbali ya vijana yanayofanyika katika mkoa wa
Ruvuma kwa kuwashawishi washiriki watembelee Hifadhi ya Msitu Asilia Matogoro.
Ninauhakika mandhari niliyoiona hapa maharusi wengi wangetamani kufika kileleni
na kufanyia sherehe zao za harusi mahali hapa.
Vilevile , Mhe. Kitandula akihitimisha ziara yake,
ameushukuru Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano unaoutoa kwa taasisi
zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii hasa kwenye kukabiliana na
changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.
Mhe. Kitandula pia alitoa rai kwa wadau wa Uhifadhi
wanaoshirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma ambao ni GIZ, Honeyguide
Foundation Tanzania, WWF na Carbon Tanzania kuona jinsi wanavyoweza kuwawezesha
askari wanyamapori wa vijiji kwa kuwapatia mitaji na kuwafundisha mbinu bora za kujiingizia
kipato; sambamba na kuendelea na majukumu yao ya kudhibiti tembo.
Wakati huo huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Rehema Madenge ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake kwa kuendelea kutoa mchango mkubwa katika kupambana na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu hususan katika wilaya za Tunduru na Namtumbo.
Na. Anangisye Mwateba- Songea Ruvuma
0 Maoni