Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.
Emmanuel John Nchimbi amewataka viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kuepuka kutoa kauli au kufanya vitendo vyenye taswira inayoweza
kutafsiriwa kuwa baadhi yao wanashabikia ukandamizaji wa haki za wananchi.
Katibu Mkuu Balozi Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa maneno na
vitendo vya wana-CCM wakati wote lazima yaakisi dhamana ambayo chama kimepewa
na wananchi ya kuwatumikia, ikiwemo kusimamia haki, bila ubaguzi wala dhuluma
ya aina yoyote.
Balozi Nchimbi amesema hayo akiwa Chuo cha Umoja wa Vijana
wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Ihemi, mkoani Iringa, alipokuwa akifungua
mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji na viongozi wa jumuiya hiyo wa ngazi za
mikoa na wilaya zote, nchi nzima, leo Alhamis, 11 Julai 2024.
“Suala jingine ninataka kuwasisitiza UVCCM ni umuhimu wa
watendaji wetu, viongozi wetu na wanachama wetu kutambua kuwa mnabeba taswira
ya Chama chetu kila wakati, katika mnayosema au kutenda. Kama kuna jambo
tunapaswa kulilinda kwa wivu mkubwa ni taswira chanya ya CCM, hasa jambo
linalohusu dhamana ya kuongoza nchi yetu na kuwatumikia wananchi kwa haki na
usawa, kwa kupinga kauli na vitendo vya ubaguzi na dhuluma kwa Watanzania,”
amesema Balozi Nchimbi na kuongeza;
“Ninyi UVCCM mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda
taswira hiyo muda wote. Tujiepushe kabisa na kauli au matendo yanayoharibu
taswira ya CCM. Katika kila unachokisema au kukitenda lazima utafakari, je kina
athari gani kwa CCM na nchi yetu.”
Aidha, katika kulinda dhima hiyo ya CCM, Balozi Nchimbi
amewakumbusha wana-CCM na Watanzania kwa ujumla kuwa hadi sasa hakuna chama
kingine tofauti na CCM kimeonesha uwezo wa kuongoza nchi na pia wananchi hawako
tayari kufanya majaribio kwa vyama vingine ambavyo havina mwelekeo, hali ambayo
ni hatari kwa uimara wa nchi.
Vilevile, Balozi amewapongeza UVCCM kwa kuweka ‘rekodi’ mpya
ya kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa walipozindua mkakati wao wa ’Tunazima Zote,
Tunawasha Kijani’, akiwataka wasonge mbele, watumie ushawishi walionao kwa
vijana nchini, kwa uaminifu na uadilifu huku wakitambua kuwa Mwenyekiti wa CCM
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan ana
imani kubwa na vijana.
Awali akimkaribisha Balozi Nchimbi, Mwenyekiti wa UVCCM
Taifa, Komredi Mohammed Ali Mohammed (Kawaida), amekishukuru Chama chini ya
Mwenyekiti wa CCM, Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi kinavyoendelea
kuwalea na kuwaamini vijana kukitumikia Chama na jumuiya zake na nchi kwa
ujumla.
Nae Katibu Mkuu wa UVCCM, Komredi Joketi Urban Mwegelo akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya mafunzo hayo, amesema yatawasaidia viongozi na watendaji wa jumuiya hiyo kwenye mikoa, wilaya na hatimae kushuka ngazi zingine nchi nzima kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi unaohitajika.
0 Maoni