Wakala ya Barbara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani
TABORA unatekeleza ujenzi wa mitaro mikubwa ya maji ili kuondoa kero kwa
wananchi hasa kipindi cha masika ambapo maji yamekuwa yakiingia kwenye makazi
ya watu.
Akiongea wakati wa ziara ya kikazi ya ukaguzi wa miradi
mkoani hapa, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia
miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila ameitaka TARURA kuhakikisha mitaro hiyo
inafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
"Kuna haja ya
kufanya matengenezo ya mara kwa mara na kufanya usafi katika mitaro hii ili
maji yapite kwa urahisi na kuondoa kero kwa wananchi kama ilivyokusudiwa,” amesema
Mhandis Mativila.
Hata hivyo Mhandisi Mativila amewataka viongozi wa Manispaa
na TARURA kuendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutunza na kusafisha
mitaro hiyo ili kuepuka mafuriko na magonjwa ya mlipuko.
Aidha, amewasihi wananchi wanaoishi karibu na mitaro hiyo
kujitolea kwa hali na mali ili kuisafisha mitaro hiyo badala ya kukaa na kuisubiri
serikali pekee.
Naye, Meneja wa TARURA Wilaya ya Tabora Mhandisi Subira Manyama amesema kuwa hadi sasa wamejenga mitaro yenye urefu mita
158 ambayo imesaidia wananchi kwa kiasi kikubwa.
"Kulikuwa na kero ya maji kuingia kwenye makazi ya watu lakini sasa kero hiyo imeondolewa ambapo mpango uliopo ni kuhakikisha tunaondoa kabisa mafuriko kwa kujenga mitaro yenye urefu wa km 25.”
0 Maoni