Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb)
mapema leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Utalii na Uchumi wa
Jamhuri ya Indonesia, Mhe. Sandiaga Salahuddin Uno ambapo wamejadiliana masuala
mbalimbali ya ushirikiano katika Sekta ya Maliasili na Utalii.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini
Barcelona Hispania, Mhe. Kairuki amesema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana
na Indonesia katika masuala ya utangazaji utalii hasa kwa kutumia njia za
kidijitali kimataifa, Uhifadhi wa wanyamapori, utoaji huduma kwa wateja na
kuvutia mikutano ya kimataifa.
Ametaja maeneo mengine ya ushirikiano kuwa ni mafunzo na
kujengeana uwezo akitolea mfano wa mafunzo ya "wellness and spa'' na
utalii wa matibabu, "Eco tourism," "Green investment" na
kuweka mkazo katika matumizi ya nishati mbadala.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka
nchini Indonesia kuwekeza nchini katika huduma ya malazi kwenye maeneo maalum
yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji ndani ya hifadhi na nje ya maeneo ya
hifadhi.
Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Uchumi wa Jamhuri ya
Indonesia, Mhe. Sandiaga Salahuddin Uno amesema kuwa Indonesia inataka
kuimarisha mahusiano baina ya nchi ya Indonesia na Tanzania na pia hivi karibuni itakamilisha mchakato wa
kusaini Mkataba wa Makubaliano (MOU).
Kikao hicho kimehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Jabir Mwadini, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania na Indonesia.
Na. Mwandishi Wetu, Barcelona-Hispania
0 Maoni