Rais Samia aviasa vyombo vya habari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri, ili kutoingiza nchi katika matatizo kutokana na kalamu zao kuwa na ncha kali.

Rais Samia ametoa wito huo leo Jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari, ambapo amewasihi waandishi wa habari kusaidia katika kudumisha amani na utulivu.

“Mwaka huu tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa nawaomba mkatumie kalamu zenu kufanya kazi zitakazojenga na sio ya kubomoa,” alisema Rais Samia na kuongeza, "Msiende kutatua nyuzi za kitambaa chetu (bedera yetu ya taifa), muache bendera yetu iendelee kupepea.”

Rais Samia pia, amevitaka vyombo vya habari nchini kuwa na uzalendo na kuacha tabia ya kubeba habari tata nyingi zilizopo hivi sasa kuhusu nchi, badala yake izifanyie kazi habari hizo na kutoa ufafanuzi ili kulitetea taifa lao.

Kuhusu madeni ya vyombo vya habari, Rais Samia ameziangiza wizara, mashrikika na taasisi za umma kuhakikisha kuwa zinafanya tathimini ya madeni yanayolipika na kuyaalipa madeni hayo yote mwisho ifikapo Desemba 24, 2024.

“Kuna madeni mengine ambayo hayana nyaraka, kuna matangazo yametolewa kwa kutumia simu hayo itakuwa ngumu serikali kuweza kuyalipa, ila madeni yote yaliyofanyiwa tathimini na yana nyaraka zote tutayalipa hivi karibuni,” aliahidi Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesisitiza mara mbili katika hotuba yake hiyo kwa kusema kuwa, “Vyombo vya habari si mshindani wa serikali bali ni mdau na mshirika muhimu wa serikali, kwa hiyo ni muhimu kuimarisha mashirikiano yao.”

Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari, linaenda na kauli mbiu ya “Jenga mustakabali endelevu kwenye sekta ya habari katika zama za kidigiti.”

Chapisha Maoni

0 Maoni