Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Nassoro Kuji ameongoza
uapisho wa Naibu Kamishna mpya wa Uhifadhi Massana Gibril Mwishawa
anayeshughulikia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara katika Shirika la Hifadhi za
Tanzania (TANAPA).
Hafla ambayo imeambatana na uvalishwaji wa cheo kipya cha
Unaibu Kamishna wa Uhifadhi imefanyika Makao Makuu ya TANAPA leo jijini,
Arusha.
Akitoa salamu za
Pongezi baada ya Uapisho huo Kamishna Kuji alisisitiza uwajibikaji na
kumtanguliza Mungu katika kutekeleza majukumu hayo ya Naibu Kamishna wa
Uhifadhi.
”Cheo huambatana na
majukumu na uwajibikaji. Hivyo basi, ni muhimu ukamtanguliza Mwenyezi Mungu
wakati wote ili aweze kukuongoza katika utekelezaji wa majukumu yako haya
mapya. Taaluma, uzoefu, umahiri na kujituma kwako, kunatupatia imani kubwa kuwa
utatekeleza majukumu yako kwa uadilifu, weledi, bidii kubwa na bila woga wala
upendeleo,” alisisitiza Kamishna Kuji.
Aidha, Kamishna Kuji aliongeza kuwa katika nafasi ya Naibu
Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Maendeleo ya Biashara kipaumbele cha
kwanza cha Shirika ni usalama wa rasilimali za Taifa na utolewaji wa huduma
bora kwa wateja wakiwemo Watalii na kusisitiza zaidi ubunifu katika mikakati
endelevu katika kuinua utalii na Uhifadhi.
”Ujitahidi wakati wote kuongeza ubunifu na kuja na mikakati
endelevu ambayo itainua sekta ya uhifadhi na utalii ili Shirika liweze
kushiriki kikamilifu katika kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada zake za makusudi za kuinua
sekta ya uhifadhi na utalii hapa nchini.”
Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Massana Gibril Mwishawa
ameishukuru Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kwa kumteua kushika nafasi hiyo ya
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara lakini pia Mhe.Dkt.Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za
makusudi anazoendelea kuzifanya katika kuinua sekta ya uhifadhi na utalii hapa
nchini.
“Mmenipa deni kubwa sana kwenu kwa watumishi wote nitakao
waongoza natambua cheo nilichovishwa leo kina majukumu makubwa ambayo
yananihitaji kuwajibika kikamilifu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za
kiuhifadhi zilizopo sasa na kuimarisha uhifadhi na utalii ndani ya shirika
ninaahidi nitaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika Hifadhi zote za Taifa,”
alisema Kamishna Mwishawa.
Bodi ya Wadhamini ya TANAPA tarehe 29.04.2024 ilimteuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi Massana Gibril Mwishawa kuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, awali kabla ya uteuzi huo alikuwa Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki akisimamia Hifadhi ya Taifa Nyerere, Mikumi, Saadani, na Milima ya Udzungwa.
Na. Edmund Salaho/ Arusha
0 Maoni