TUME ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) chini ya
ufadhili wa Benki ya Dunia, inaendelea na utekelezaji wa hatua za awali za
upembuzi yakinifu wa mabwawa sita ya umwagiliaji kwaajili ya kunusuru mradi wa
reli ya kisasa (SGR).
Lengo ni kukabiliana na mafuriko na kulinda mradi wa Reli ya
Kisasa (SGR).
Mabwawa hayo yanajengwa katika maeneo ya Kidete mkoani
Morogoro na Kimagai, Dabalo, Hombolo, Ikowa na Buigiri yaliyopo mkoani Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond
Mndolwa, akiwa ameongozana na wataalamu kutoka Shirika la Reli nchini, wataalamu
wa Tume pamoja na wataalamu wa Benki ya Dunia na wale wa Bonde la Wami Ruvu
wakati wa kufanya ziara ya matayarisho
ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu amesisitiza umuhimu wa mradi huo kwa kuwa
mabwawa hayo yataimarisha usalama wa mradi wa SGR.
Mndolwa amesema timu hiyo ya wataalamu wametembelea mradi wa
bwawa la Kidete mkoani Morogoro na bwawa
la Membe, Msagali, Kimagai, Hombolo na Dabalo mkoani Dodoma, kwa lengo la
kujionea hali halisi ya mabwawa hayo.
“Utekelezaji wa
miradi hiyo ya mabwawa unalenga kuvuna maji ya mvua ili kuzuia mafuriko kwenye reli ya kati sambamba na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji
mkoani Morogoro na Dodoma,”alisema.
Mradi huo wa kukabiliana na mafuriko, unahusisha ujenzi wa
mabwawa mapya pamoja na ukarabati wa mabwawa yaliyokuwepo awali ambayo ni bwawa
la Hombolo na Dabalo.
Katika hatua nyingine wataalamu wa Tume ya Taifa ya Uwagiliaji
(NIRC) wamewezeshwa kupata mafunzo juu ya usalama na matayarisho ya ujenzi wa
mabwawa hayo ikiwa ni miongoni mwa hatua za awali katika utekelezaji wa mradi
wa ujenzi na ukarabati wa mabwawa hayo.
Lengo ni kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kwa ufanisi na
kuwezesha kuvuna maji, kuzuia mafuriko na kulinda reli ya kati katika mikoa ya
Dodoma na Morogoro.
Mafunzo hayo yametolewa jijini Dodoma na wataalamu kutoka
Benki ya Dunia kwa lengo la kuwakumbusha wataalamu wa Tume kuzingatia usalama
wa mabwawa katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi, ili kuepusha madhara
yanayoweza kutokea ikiwemo vifo na uharibifu wa makazi na miundombinu mingine.
Katika mafunzo hayo wataalamu hao wamepatiwa elimu ya
kutambua viashiria vya hatari kwa upande wa mabwawa pamoja na namna bora ya
kujiandaa ili kupunguza au kukabilina na
madhara yanayoweza kutokea ikiwa mabwawa yatakoyojengwa na yanayoendelea
kujengwa, yataonesha dalili zozote za hatari.
Vilevile, wataalamu hao wamekumbushwa kuhusu sera na sheria
za mabwawa; kutoka kwa wataalamu wa Wizara ya Maji, ikiwemo umuhimu wa
kuzingatia lengo la serikali la kujenga
uwezo wa usalama wa mabwawa utakaosaidia
miundombinu hiyo kudumu kwa muda mrefu zaidi.
Benki ya Dunia imedhamiria kuunga mkono kwa dhati ujenzi wa SGR nchini Tanzania. Mradi huu wa reli unaolenga kubadilisha miundombinu ya usafiri unakwenda kufungua njia ya usafiri wa kisasa wa reli ya umeme, kuunganisha mikoa muhimu ndani ya nchi na nchi jirani. Ili kulinda SGR kutokana na mafuriko, Benki ya Dunia inashirikiana na TRC, NIRC, na Wizara ya Maji ambapo Wadau hawa kwa Pamoja, wamejidhatiti kushikirikiana katika ujenzi wa mabwawa ya kukusanya maji ya mvua, kwa namna itakayo imarisha usalama wa SGR; pamoja na kuwezesha upatikanaji wa maji yatakayo tumika kwa matumizi ya binadamu, wanyama, uvuvi pamoja na kilimo cha Umwagiliaji.


0 Maoni