Waziri Kairuki azitaka nchi za AFR100 kujikita katika kuongoa misitu iliyoharibiwa

 

Waziri wa Maliasili wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ametoa wito kwa nchi wanachama wa Mkakati wa Kuongoa Ardhi na Misitu iliyoharibiwa takribani Hekta milioni 100 Barani Afrika (African Forest Restoration Initiatives - AFR100), kuweka mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya kielektroniki kuhakikisha  lengo la kuongoa misitu hiyo linafikiwa kwa kuona uhalisia wa utekelezaji wa mkakati wa kuongoa misitu iliyoharibiwa.

Ameyasema hayojana jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 8 wa Mwaka wa nchi 34 za Afrika Wanachama  katika Mkakati wa Uongoaji wa Ardhi na Misitu iliyoharibika.

“Naomba kupendekeza kwamba ni muhimu kuweka mifumo wa ufuatiliaji na urejeshaji wa misitu na mifumo ya uwajibikaji ili tuweze kuona hali halisi ya kinachoripotiwa katika maeneo husika kuhusu urejeshaji wa misitu,” Mhe. Kairuki amesisitiza na kuongeza kwamba Tanzania imeanza kuangalia namna ya kuweka mfumo hiyo ili kuweza kufuatilia, kurahisisha upatikanaji wa taarifa.

Ameongeza kuwa katika kutekeleza mpango huo wa kurejesha misitu, Tanzania imefanikiwa kurejesha hekta milioni 2.4 kupitia afua za upandaji miti, ambayo ni sawa na asilimia 46.3 ambapo iliahidi kurejesha hekta milioni 5.2 za misitu na mandhari kwa mwaka 2018.

“Ili kudhihirisha nia thabiti ya Serikali ya utekelezaji wa mkakati wa kuongoa misitu nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliongoza kampeni ya upandaji miti katika siku yake ya kuzaliwa mwaka 2023 kijijini kwao Kizimkazi Zanzibar ambapo zaidi ya miti 1,500 ilipandwa katika siku hiyo, lakini kampeni ya upandaji miti iliendelea kwa mwezi mzima ambapo miti takribani milioni 8.3 ilipandwa,” Mhe. Kairuki alibainisha.

Amesema kuwa Rais Samia amekuwa kinara Barani Afrika na duniani katika kuhakikisha misitu inaongolewa na kutunzwa hasa kupitia  kampeni yake ya nishati safi ambapo ameendelea kuhamasisha nchi nyingine duniani kutoa ahadi za kuhakikisha zinalinda misitu na zinaweka afua mbalimbali za kulinda misitu.



Chapisha Maoni

0 Maoni