Mchezaji wa kimataifa wa soka kutoka Morocco anayechezea
timu ya PSG, Archraf Hakimi leo ametoa
msaada wa vifaa mbalimbali kwa
wanafunzi zaidi ya 400 wenye uhitaji
maalum kwenye shule ya Sekondari ya Patandi ya jijini Arusha vyenye gharama ya
zaidi ya bilioni moja.
Baadhi ya vifaa hivyo ni pamoja na komputa zaidi ya 50, samani,
vifaa maalum alama nundu, Mashine za kuchomea taka na kuchemshia maji.
Katika hafla hiyo ambayo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.
Angellah Kairuki alikuwa mgeni rasmi ambapo aliwakilishwa na Katibu Mkuu wa
Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi mchezaji huyo ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa zinazofanyika katika kutoa huduma za
elimu kwa watoto wenye uhitaji maalum.
Mchezaji huyo ambaye ni mara yake ya kwanza kutoa misaada
kupitia taasisi yake nje ya nchi ya Morocco ameuhakikishia Serikali kuwa
ataendelea kushiriki kikamilifu kutoa misaada kwa jamii hapa nchini.
Aidha, Hakimi ambaye ameletwa nchini kwa mwaliko maalum wa
Rais wa Yanga Mhandisi Hersi Said amesema amevutiwa na vivutio vya Utalii na
kuahidi kuja tena.
Hakimi ni miongoni mwa wachezaji nguli duniani ambaye
anawafuasi zaidi ya milioni 20 duniani pia ameshukuru Yanga, Wizara ya
Maliasili na Utalii na Bodi ya Utalii kwa uratibu mzuri wa ziara yake.
Kwa upande wake Dkt. Abbasi amemshukuru Hakimi kwa misaada
yake na Mhandisi Hersi kwa kusaidia
kuleta watu mashuhuri kama Hakimi ambao wanashaidia kutangaza utalii wa
Tanzania na kutoa wito kwa watu wengine kufanya hivyo.
"Nakumbuka siku ambayo
Injinia ulikutana na Hakimi Paris
ulinipigia simu kuwa una "surprise" na ukasema tunataka kumletea
Hakimi nikasema sawa kabisa mlete," amefafanua Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi ameendesha harambee ya kuchangia shule
hiyo ambapo Klabu ya Yanga imetoa vitanda 40 na magodoro yake, na wadau wengine
ambao waliweza kutoa zaidi ya milioni mbili na laki sita na ahadi ya milioni 3.
Injinia Hersi amempongeza Mkuu wa shule ya Sekondari ya
Patandi kwa ufanyaji kazi wake ambapo pia amefafanua kuwa wazo la kuichagua
shule ya Sekondari ya Patandi lilitoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe
Angellah Kairuki.
Katika hafla hiyo wizara imeweza kumpatia zawadi Hakimi, Rais wa Yanga na Mkuu wa shule ya Sekondari ya Patandi Janeth Mollel kabla ya Hakimi kucheza mpira na vijana wafuasi wa Yanga.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas (kutosho) akimkabidhi zawadi ya picha iliyochorwa wanyama Mchezaji wa Club PSG ya Ufaransa na timu ya Taifa ya Morocco Achiraf Hakimi. Mchezaji huyo mashuhuri duniani alikuwa na ziara ya kutembelea vivutio vya Utalii katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti.
Na John Mapepele- Arusha
0 Maoni