Wananchi wa Kata ya Kakola na Ikomwa, Manispaa ya Tabora
wameishukuru serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)
kwa kuwafungulia mawasiliano ya daraja katika barabara ya Kakola - Mwibiti.
Daraja hilo liliharibiwa na mvua za Elnino zilizonyesha
msimu wa masika mwaka huu.
Wakiongea kwa wakati tofauti Diwani wa Kata ya Kakola Mhe.
Chota Lukuiza amesema kuwa kutokana na mvua kubwa za mwaka huu eneo hilo
lilikumbwa na mafuriko na kusababisha wananchi wake kushuka kiuchumi.
“Tunamshukuru na kumpongeza
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za ujenzi wa barabara
hii, mvua ya kipindi hiki ilisababisha kukata mawasiliano kwa kata hizi mbili
lakini bado ametuletea fedha za dharura na kuweza kujenga ‘Box Kalvati’ na kalvati
zingine pamoja na kuinua barabara hii.”
Ameongeza kusema kwamba kutengamaa kwa barabara hiyo
inapelekea uchumi wa wananchi wa kata hizo kukua kwani sasa hivi wananchi
wanaweza kupita wao wenyewe na kupitisha
mazao yao ya biashara.
“Barabara hii ni sehemu kubwa ya uchumi wa wakazi wa kata
hizi pia ni kiunganishi cha wilaya ya Uyui na Nzega ambapo hutumika kusafirisha
mazao yao ya biashara kutoka mashambani.”
Naye, Mtendaji wa kijiji cha Ikomwe Bw. Abasi Baluguza
amesema wakati wa mafuriko shughuli zao za kiuchumi zilisimama na baadhi ya
wananchi ilibidi wazunguke umbali mrefu ili kuweza kufika mjini ambapo ilikuwa
gharama kubwa na pia walitumia muda mrefu.
“Kwa kweli jambo ambalo limeshughulikiwa na TARURA,
tunamshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuliona hili kwani hivi sasa kijiji chetu cha
Ikomwe kimefunguka.”
Amesema awali maji yalikuwa mengi sana na wanamshukuru Mungu
kwani hakukutokea vifo zaidi ya wananchi kusitisha shughuli zao za kiuchumi,
hivyo wanashukuru kwa ujenzi wa ‘Box kalvati’ na barabara hiyo kwa ujumla.
Wakati huo huo Mkazi wa kijiji cha Magowelo Kata ya Kakola
Bi. Pili Nasoro amesema kwamba adha kubwa iliwapata wananchi wa vijiji hivyo
hususan wajawazito na wanafunzi kutoka vijiji vya karibu ambao hupata huduma
katika zahanati na shule za msingi na sekondari zilizopo kata ya Ikomwa.
“Yaani hapa ilikuwa ni bahari, wanafunzi wetu na wajawazito
walikuwa wanapata shida, kakini tunamshukuru sana Mama Samia Rais wetu kwa
kutuwezesha kurudisha mawasiliano sisi wana Kakola hatuna cha kumlipa kwani
sasa tunaweza kwenda kliniki na hata wakulima wanaweza kupeleka bidhaa zao
sokoni”.
Kaimu Meneja wa TARURA wilaya ya Tabora Mhandisi Gwalugano
Mwamwifu amesema kutokana na mvua za
mwaka huu barabara nyingi ziliathiriwa na mvua hizo na moja ya maeneo waliyorudisha
mawasiliano ni barabara hiyo ya Kakola-Mwibiti ambapo wameweza kurudisha
mawasiliano kwa 100%.
Amesema kazi iliyofanyika ni ujenzi wa ‘Box Kalvati’ yenye urefu wa mita 10, Kalvati laini 5, kuchimba mitaro Km. 3 kwaajili ya kupeleka maji kwenye kalvati pamoja na kuinua tuta la barabara lenye urefu wa Km. 7 ambayo iliathiriwa na mvua.
0 Maoni