Wasimamishwa kazi na RC Makonda kwa kutafuna milioni 600

 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda, amewasimamisha kazi Mganga Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha Dkt. Petro Mboya pamoja na watumishi wengine wa idara ya Afya Wilayani humo ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Milioni 600 zilizokuwa zitumike kwenye sekta ya afya.

RC Makonda ameetoa agizo hizo hilo wakati wa mkutano wake wa hadhara eneo la Ngaramtoni Jijini Arusha baada ya kubaini kuwa Watumishi hao bado wanaendelea na kazi wakati uchunguzi ukiendelea dhidi yao.

Katika hali ya kustaajabisha, RC Makonda ameshangazwa na Jeshi la Polisi Wilayani Arumeru kwa kushindwa kumpata Mhasibu msaidizi wa Halmashauri ya Arumeru anayedaiwa kutoroka na kutoonekana ofisini mara baada ya kudaiwa kuiba Milioni 333 za serikali.

RC Makonda, amewaambia wananchi wa Arumeru kuwa Halmashauri yao imeoza na inanuka rushwa katika idara mbalimbali na hivyo ametangaza kuandika barua serikali kuu kuomba kuongezewa nguvu kwenye Taasisi ya  kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Arusha ili kupambana na vitendo vya rushwa alivyosema vimekithiri kwenye Mkoa wa Arusha.

Aidha, RC Makonda ameapa kupambana na rushwa kwenye Mkoa wa Arusha na ametahadharisha kwa watumishi na viongozi wengine wenye kuendekeza vitendo vya rushwa akisema siku zao za moto zimekaribia.

Chapisha Maoni

0 Maoni