Serikali yasikia kilio cha wananchi cha kifuta machozi na kifuta jasho

 

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesikia kilio cha muda mrefu cha Wananchi wanaodhuriwa na Wanyama wakali na waharibifu akiwemo Tembo kwa kuboresha viwango vya kifuta jasho na kifuta machozi kutoka shilingi milioni moja hadi milioni mbili kwa mwananchi atakayepoteza uhai, shilingi laki tano hadi milioni moja kwa ulemavu wa kudumu na kutoka shilingi laki mbili hadi laki tatu kwa majeraha ya muda mfupi.

Akizungumza katika Semina ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuwajengea uelewa wabunge hao kuhusu namna Wizara inavyoshughulikia changamoto mbalimbali zinazosababishwa na Wanyama wakili na waharibifu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Anjellah Kairuki amesema Serikali imefanya maboresho ya kanuni za fidia za mwaka 2011 si kwa binadamu tu bali hata kwa upande wa mazao ambapo kwa sasa Mwananchi atalipwa kifuta jasho cha shilingi laki moja na nusu kutoka shilingi 37 elfu za awali kwa heka kwa kuzingatia umbali wa shamba kutoka hifadhini.

Mhe. Kairuki amewaomba Wabunge hao kuwahamasisha watendaji wa Halmashauri kuwasilisha wizarani kwa wakati taarifa za matukio ya mauaji, majeruhi au uharibifu wa mashamba unaofanywa na wanyamapori walioanishwa kisheria kulipiwa fidia ili kuwezesha mchakato wa malipo kufanyika kwa wakati na kuondoa malalamiko ya ucheleweshaji wa malipo kwa wananchi walioathirika.

Akizungumza wakati akijibu baadhi ya hoja za Wabunge hao, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dastan Kitandula amesema mbali na madhara yanayosababishwa na Tembo lakini pia Mamba ni mmojawapo ya Wanyama wanaosababisha vifo na ulemavu kwa baadhi ya wananchi hivyo Wizara ipo katika mchakato wa kutambua maeneo ambayo matukio ya binadamu kushambuliwa na mamba yanajitokeza mara kwa mara hususani wakati wa kuteka maji tofauti na matukio yanayotokea wakati wa uvuvi ili kuanzisha mfumo wa kutumia vizimba itakayosaidia kupunguza matukio hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava amesema Wabunge wanatambua jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kutatua changamoto ya madhara yanayosababishwa na wanayama wakali na waharibifu na kutaka jitihada zaidi na tafiti za kisayansi ziendelee kufanyika ili kupata suluhu ya kudumu ya tatizo hilo.

Amesema hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Maliasili ya kutengeneza vifaa mbalimbali vya kufukuza Tembo ikiwemo Mabomu, mizinga ya nyuki na utoaji wa elimu kwa kiasi kikubwa imesaidia kupunguza madhara kwa wananchi na kuomba kutengwa kwa bajeti ya kutosha ili vifaa hivyo vitengenezwe kwa wingi na kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini.

Wakichangia katika Semina hiyo baadhi ya Wabunge wameomba kusogezwa kwa ukaribu huduma ya maafisa wanyamapori katika maeneo ya wananchi kwa kujenga ofisi ndogo za maafisa wanayamapori wenye vifaa na ujuzi wa kuwafukuza wanayamapori hususani Tembo pindi wanapovamia makazi na mashamba ya wananchi hususani katika maeneo yanayozunguka hifadhi za Taif ana mapori tengefu.

Na. Emmanuel Buhohela

Chapisha Maoni

0 Maoni