Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.
Hussein Ali Mwinyi ametoa wito na kuwakaribisha wafanyabiashara kutoka Ufaransa
kuangalia fursa kuwekeza Zanzibar katika maeneo mbalimbali.
Rais Dk. Mwinyi amesema hayo alipofungua Mkutano wa majadiliano
ya fursa za uwekezaji kati ya Ufaransa na Zanzibar kutoka kwa ujumbe wa
Wafanyabiashara wa makampuni 20 ya Ufaransa katika ukumbi wa Hoteli ya Park
Hyatty Zanzibar tarehe: 29 Mei 2024.
Aidha Rais Dk.Mwinyi amesema sera kuu ya uchumi wa Zanzibar
ni uchumi wa buluu hivyo amewakaribisha kuangalia fursa za kuwekeza katika
sekta ya utalii wa fukwe, urithi,
michezo na mikutano, sekta ya bandari,
mafuta na gesi, sekta ya bandari
ikiwemo ya makontena , uvuvi pamoja na meli za usafirishaji wa mizigo na
abiria.
Pia amebainisha fursa za miradi ya miundombinu ikiwemo
barabara, viwanja vya ndege , sekta ya nishati na maji, pamoja na kilimo cha
viungo.
Rais Dk. Mwinyi amewahikikishia wawekezaji hao kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mazingira mazuri kikamilifu ya kufanya
biashara na uwekezaji.
Ujumbe huo pia uliambatana na Balozi wa Ufaransa nchini
Tanzania Mhe.Nabil Hajlaoui, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe.Ali Mwadini
na Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la MEDEF kutoka Ufaransa, Gerald Wolf.
Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri na sekta binafsi wameshiriki mkutano huo.
0 Maoni