Jitahidi za Serikali za kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya Hifadhi na wananchi zinaendelea kuzaa matunda baada ya kutatua mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 20 baina ya Pori la Akiba Liparamba lililopo Mkoani Ruvuma na vijiji vitano vinavyozunguka hifadhi hiyo.
Hayo yamebainika jana Mei 28, 2024 katika ziara ya kuelezea
namna TAWA ilivyotekeleza kikamilifu maagizo ya Serikali na mapendekezo ya
Baraza La Mawaziri la Kisekta (BLM) kuhusiana na utatuzi wa mgogoro huo.
Akizungumzia mgogoro huo, Kamanda wa Hifadhi hiyo Annzikar
Joseph Lyimo amesema Pori la Akiba Liparamba lilikuwa na mgogoro wa mipaka kati
yake na vijiji vinavyolizunguka ambavyo ni Ndondo, Mseto, Mipotopoto, Liparamba
na Mitomoni. Mgogoro unaotajwa kudumu zaidi ya miaka 20 lakini ulitatuliwa
Mwaka 2023 ikiwa ni matokeo ya ziara ya
Mawaziri wa Wizara nane wa kisekta ya kutembelea maeneo yenye migogoro ya
matumizi ya Ardhi likiwemo Pori hilo ambapo walitoa maelekezo ya kupitia upya
kwa mipaka na hatimaye maelekezo hayo kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Aidha, amesema zoezi la utatuzi wa mgogoro husika lilikuwa
shirikishi kwa kufanya vikao mbalimbali vilivyohusisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nyasa pamoja na
wananchi ambapo wananchi wa
vijiji husika waliteuliwa katika zoezi zima la uwekaji vigingi na kufanikiwa kujenga jumla ya vigingi 140
kuzunguka hifadhi hiyo.
Akizungumzia hatua hiyo, mkazi wa Kijiji cha Liparamba Bw.
Eligius Simon Mbawala ambaye pia alikuwa fundi wa kujenga vigingi aliyeteuliwa
na wananchi wenzake kushirikiana na wahifadhi katika zoezi zima la kuweka
vigingi katika hifadhi ya Liparamba ameeleza namna zoezi hilo lilivyokuwa
shirikishi.
"Tumemaliza mgogoro huu mimi nikiwa fundi nimezunguka
Pori zima la Liparamba ukianzia mpaka wa mitomoni hadi ndondo yote nimepita
kuzunguka na kujenga hizo "beacon" (vigingi),..mpaka tulipo hapa leo
tunafurahi, na tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini
ya Mama Samia kwa kumaliza huu mgogoro vizuri na watu sasa wanaendelea kufurahi
na kunufaika na maeneo haya kwa kazi zao za kiuchumi na maendeleo ya kijamii
kwa ujumla, " amesema.
Kwa upande wake Afisa Habari
wa TAWA Beatus Maganja amesema pamoja na maelekezo mengine, Serikali ilitoa maagizo kwa Mamlaka zote
zinazohusiana na Hifadhi nchini kushirikisha wananchi katika maeneo yote ili
kuwe na mapitio ya pamoja ya mipaka ili kila mwananchi ajue mpaka uko wapi, na
pia kuweka vigingi kama alama inayoonesha pande zote mbili.
0 Maoni