WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya imedhamiria
kuongeza ushiriki wa wananchi katika kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza kipato
kwa wananchi wengi na kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii mijini na
vijijini.
“Ili kufikia lengo hilo, Serikali inatekeleza Mpangokazi wa
Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini kwa kufanya mapitio na
maboresho ya sera, sheria na kanuni ambazo zinakuwa ni kikwazo katika ufanyaji
wa biashara nchini.”
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei 23,
2024) kwenye ufunguzi wa Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji baina ya
Uganda na Tanzania, katika Hoteli ya Johari Rotana jijini, Dar-es-Salaam.
Amesema Serikali imeirisha utoaji huduma kwa imeunganisha
mifumo ya kielektroniki 55 ya taasisi 50, pia sheria 13 zimeshafanyiwa
marekebisho ili kupunguza au kuondoa kodi, ada na tozo na kupunguza au kuweka
misamaha ya ushuru wa forodha.
“Mifumo hiyo imeunganishwa ili kubadilishana taarifa na
kukamilisha uundaji wa mfumo wa kielektroniki wa dirisha moja la utoaji huduma
kwa wawekezaji (Tanzania Electronic Investiment single window).”
Amesema mbali na maboresho ya mifumo, Serikali imeendelea
kuimarisha nidhamu katika utendaji kazi, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za
umma, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji
biashara na uwekezaji.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutoa ahueni za
kikodi kwa wawekezaji katika viwanda vya ndani na kuanza utekelezaji wa mpango
wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara Tanzania (Blueprint Regulatory
Reforms to Improve the Business Environment for Tanzania).
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka
mazingira wezeshi kwa ajili ya kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vinavyotumia
malighafi za ndani kutoka sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, madini na maliasili.
Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa jumla ya kampuni mpya 15
zenye mitaji ya Dola za Marekani milioni 215.48 zinazojishughulisha na
uchakataji wa mazao ya kilimo na madini zimesajiliwa na kupewa leseni.
“Kutokana na jitihada mbalimbali, Serikali imewezesha
uanzishaji wa viwanda 332 vya kimkakati na kurejesha viwanda 20
vilivyobinafsishwa. Tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua ya kugawa viwanda
hivyo ambapo, EPZA wamepewa viwanda
nane kwa ajili ya kuviendeleza, NDC na
SIDO wamekabidhiwa viwanda viwili na viwanda kumi vilivyobaki bado vinatafutiwa
wawekezaji wapya.”
Amevitaja viwanda hivyo kuwa ni Mbeya Ceramics Company Ltd, Nachingwea Cashewnuts
Processing Factory, Mafuta Ilulu Ltd, Mkata Sawmills Ltd, Tanganyika Packers
Limited (TPL) Shinyanga Plant, Mwanza Tanneries Ltd, Mang’ula Mechanical and
Machine Tools, National Steel Corporation, pamoja na Mbeya Meat Processing
Plant.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka Tumieni Makongamano haya kubaini fursa za uwekezaji wa pamoja kati ya wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi zetu ikiwa ni pamoja na kuweka bayana faida zinazotokana na uwekezaji wa pamoja. “Ikiwezekana andaeni maonesho ya fursa hizi ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi zetu.”
0 Maoni