WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi
wafuatilie mienendo ya watoto wao waendapo shuleni ikiwemo na mahudhurio na
masomo yao darasani.
“Serikali inaendelea kuimarisha mahudhurio ya watoto shuleni
kwa kuzungumza na wazazi ili kuhakikisha kila mzazi anasimamia mahudhurio ya
mtoto wake, kwenda shule, kuingia darasani, lakini anaporudi nyumbani, mzazi
afuatilie mwenendo wa masomo ya mtoto huyo ili ajiridhishe kama kweli mtoto
alikwenda shuleni.”
Ametoa wito huo Bungeni leo (Alhamisi, Mei 23, 2024) wakati
akijibu swali la Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda kwenye kipindi cha maswali
ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alihoji Serikali ina mkakati gani wa
kuhakikisha wanafunzi wanaoanza masomo wanamaliza wote shule ukiacha wale ambao
hufariki dunia.
Katika ngazi ya shule za sekondari, Waziri Mkuu amesema:
“Tunaimarisha ujenzi wa mabweni na hosteli kwaajili ya wanafunzi wa kike na wa
kiume ili wasome palepale, walale pale, wacheze pale lakini pia usimamizi wa
maadili yao uweze kuimarika.”
Amesema maelekezo yalikwishatolewa kwenye Halmashauri zote
za Wilaya kwani ndizo zinasimamia shule za msingi na sekondari na kwenye ngazi
za mikoa ili wafanye ufuatiliaji shuleni. “Pia tumeimarisha taasisi yetu ya
Uthibiti Ubora ambayo moja ya majukumu yake ni kuhoji idadi ya wanafunzi
waliosajiliwa, waliopo darasani na wanatakiwa wahoji ni kwa nini wengine hawapo
kulingana na usajili uliopo.”
“Tunaamini kupitia hatua hizi, utoro utapungua na tutaanza
kuona wanafunzi waliosajiliwa wanafikia asilimia 95 hadi 98 ya wanaomaliza.”
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi walioacha masomo
kwa sababu mbalimbali wanarejeshwa shuleni ili waweze kutimiza ndoto zao.
“Ninampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi
chake cha uongozi alielekeza wanafunzi wa kike waliochishwa masomo warudi
shuleni ili waweze kutimiza ndoto zao.”
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Asia Abdukarimu
Hamlanga, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo
kupitia maboresho ya Sera ya Elimu yanayofanyika sasa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewashukuru wananchi
wanaoishi kandokando ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria na kwamba Serikali
inatambua mchango walionao katika kulinda maeneo hayo.
Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi
wanaoishi kwenye maeneo hayo, pia inaweka alama katika mipaka iliyowekwa kisheria.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na Kamati za Mazingira za kila kijiji
juu ya uhifadhi, ulinzi wa mipaka na tunawapa nguvu ya kusimamia maeneo hayo.”
“Nitoe wito kwa wahifadhi wote wanaolinda maeneo
yaliyohifadhiwa, wajenge mshikamano na wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo
kwa kujenga tabia ya kufanya mazungumzo na Serikali za vijiji zilizoko kwenye
maeneo hayo,” amesisitiza.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge Viti Maalum, Stella Simon Fiyao ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa umma ili wananchi wote wawe sehemu ya kulinda maeneo ya hifadhi na kuepusha migogoro na wahifadhi.
0 Maoni