Tanzania yaungana na nchi wanachama wa Shirika la Miliki
Ubunifu Duniani (WIPO) kupitisha na kusaini Mkataba wa kihistoria wa kimataifa
kuhusu Miliki Ubunifu, Rasilimali za Kijenetiki na Maarifa ya Jadi.
Mkataba huo unalenga kulinda haki za wenyeji asilia na jamii
za kijadi katika kuhakikisha matumizi ya rasilimali za kijenetiki na maarifa ya
jadi katika tafiti na vumbuzi yanaleta faida kwa jamii hizo.
Mkataba huo wa kihistoria na wa aina yake umejadiliwa kwa
takribani miaka 25 na nchi wanachama wa WIPO kabla ya kupitishwa rasmi tarehe
24 Mei, 2024 katika Mkutano wa Kidiplomasia uliofanyika katika Makao Makuu ya
Shirika hilo Jijini Geneva, Uswisi.
Mheshimiwa Dkt. Abdallah S. Possi, Balozi na Mwakilishi wa
Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa Jijini
Geneva aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa Kidiplomasia
uliopitisha Mkataba tajwa, na kusaini Mkataba kwa upande wa Tanzania.
Walioshuhudia hafla ya utiaji saini mkataba huo ni Bw.
Godfrey Nyaisa, Afisa Mtendaji wa BRELA, Bw. Twalib Njohole, Msajili wa
Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea kutoka Wizara ya Kilimo,
Bi. Loy Mhando, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA na Bi. Zulekha Fundi,
Afisa Mambo ya Nje kutoka Ubalozi wa Tanzania Geneva.
Baada ya Mkataba huu kuridhiwa na nchi, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni
(BRELA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) watakuwa na jukumu
la kuhakikisha waombaji wa ulinzi wa Vumbuzi kupitia Sheria za Hataza
wanafichua taarifa za mahali zilipopatikana rasilimali za kijenetiki na maarifa
ya jadi yaliyotumika katika tafiti na vumbuzi husika.
Vilevile, kufuatilia matumizi ya rasilimali hizo
zinazopatikana hapa nchi ambazo watafiti na wavumbuzi kutoka nchi nyingine
wanazitumia katika tafiti na vumbuzi zao ili kuhakikisha wamiliki wa rasilimali
hizo hapa nchini wanapata faida zitakazotokana na matumizi ya rasilimali hizo.
Mkataba huu utaanza kutumika rasmi siku 30 baada ya nchi 15 kuwasilisha nyaraka za uridhiwaji wa Mkataba huo katika Ofisi za WIPO.
0 Maoni