Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewaasa Watanzania kutumia fursa ya wasaidizi wa msaada wa kisheria ili
kupata huduma za kisheria na kutatua migogoro inayowakabili katika maeneo yao.
Akizungumza leo Mei 26, 2024 Mkoani Njombe katika hafla ya
uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Dkt. Biteko amesema
kuwa Serikali iliamua kuandaa Kampeni hiyo ili kusaidia wananchi wasio na uwezo
wa kumudu gharama za kisheria kupata huduma hizo bila malipo na kutatua
changamoto zao.
“Serikali imeandaa na itawaletea wataalamu wa msaada wa
kisheria wenye uwezo wa kusaidia wananchi katika changamoto zenu hivyo wananchi
wa Njombe na Watanzania kwa ujumla mtakapofikiwa na kampeni hii katika maeneo
yenu tumieni fursa hii kupata huduma za kisheria na kutatua migogoro,” amesema
Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa ili kuwa na
jamii ya watu wenye kuelewana ni muhimu kutatua migogoro mapema ili
kuepusha madhara yanayosababishwa na migogoro hiyo ikiwemo visasi.
"Mhe. Rais amekuwa akisisitiza maridhiano na tutatue changamoto zetu bila kumuonea mtu, tuheshimu vyombo vya sheria katika maamuzi yetu,”amefafanua.
Aidha, Dkt. Biteko amewataka wasaidizi wa msaada wa kisheria kuhudumia wananchi kwa kusikiliza
kero na migogoro inayowakabili kwa upendo huku akiitaka Wizara ya Katiba na
Sheria kutekeleza jukumu la kusaidia wananchi kupata huduma za sheria kwa
kuimarisha matumizi ya mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
ili wananchi wasisafiri umbali mrefu kutafuta haki.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa migogoro mingi inaanzia
ngazi ya jamii, hivyo viongozi ni muhimu kushiriki kikamilifu katika Kampeni
hiyo ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
“Migogoro hii isipotatuliwa inaleta athari kwa watoto na
jamii kwa ujumla ambapo hadi sasa migogoro 516 imepatiwa ufumbuzi na endapo
ingeachwa ingesababisha madhara makubwa kwa watu wengi," amebainisha Dkt.
Biteko.
Kupitia hafla hiyo, Dkt. Biteko amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa
Njombe, Mhe, Anthony Mtaka kusadia mashirika ya wasaidizi wa msaada wa kisheria
kupatiwa ofisi ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuhakikisha wananchi wa Njombe
wanasikilizwa katika changamoto zao za utatuzi wa migogoro.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi
Pindi Chana amesema kuwa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi ni njia muhimu ya kuwawezesha
kutumia muda wao kujiletea maendeleo badala ya kuendeleza migogoro.
"Mhe. Rais Samia amekuwa akisikiliza kero za wananchi
akiwa katika ziara zake na kampeni hii ya msaada wa sheria ni utekelezaji wa
Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Mhe. Rais ametuelekeza tuwasikilize wananchi na
kujua kero zao ili tuweze kuwasaidia kuzikutatua na kuwapa msaada wa kisheria,”amesema
Balozi Chana.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Mhagama amesema kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni sehemu ya mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali “Sisi kama Kamati tumeshiriki katika mchakato wa upatikanaji wa bajeti wa kutekeleza shughuli hii tunaona dhamira ya dhati ya Mhe. Rais ya kusogeza huduma ya kisheria kwa wananchi na tunampongeza Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuendelea kutekeleza jukumu hili,” amebainisha Mhe. Mhagama.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni