Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango
wa madhehebu ya dini katika kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali nchini.
Amesema kuwa Serikali
imekuwa ikishirikiana na Sekta binafsi zikiwemo Taasisi za dini katika kutoa
huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa kwa kuwa maendeleo ya nchi hayawezi
kuimarika bila ushirikiano na ushirikishwaji wa kila mtu.
Amesema hayo leo
(Jumapili Mei 26, 2024) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye
ibada ya kuwekwa wakfu kwa askofu msaidizi wa jimbo kuu katoliki Mbeya
Mshashamu Godfrey Jackson Mwasekaga na Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji
jimbo kuu la Mbeya, iliyofanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Ibada
hiyo imeongozwa na Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycap Cardinali Pengo.
“Ni ukweli
usiopingika uwepo wa Taasisi za Dini unasaidia katika kuchangia juhudi za
Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kama vile elimu, afya, kilimo, maji na
fedha, huduma ambazo Serikali peke yake isingeweza kuzifikisha kwa wananchi
mara moja”.
Aidha, Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalipongeza kanisa
Katoliki kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuunga mkono juhudi za
Serikali kwenye kuimarisha utoaji na upatikanaji wa huduma bora za jamii kwa
Watanzania.
“Hapa Mbeya na Mkoani
Songwe ninafahamu kuwa Jimbo Kuu
Katoliki la Mbeya linashirikiana na Serikali katika kutoa huduma afya katika
maeneo 15 ya kutolea huduma ikiwemo Hospitali mbili za Igogwe iliyoko
Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe na Mwambani iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya
Songwe, Vituo vya Afya vitatu (viwili Mkoa wa Mbeya na kimoja Mkoa wa Songwe);
Zahanati 10 (7 zipo Mkoa wa Mbeya na 3 Mkoa wa Songwe)”
Pia, amewakikishia viongozi wa dini kuwa Serikali iko tayari
kushirikiana na madhehebu yote ya dini pamoja na wadau wote katika kuhakikisha
huduma bora za afya na elimu hapa nchini zinapatikana
adhalika Waziri Mkuu
ametoa wito kwa viongozi wa dini waendelee kuweka msisitizo katika masuala ya
kuwekeza katika vijana na kukemea vitendo vyote hatarishi kwa vijana mfano
matumizi ya dawa za kulevya, wizi, ubakaji na kadhalika.
Amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi na majukumu
makubwa ya viongozi wa madhehebu ya dini ya kuwaongoza watu kiroho kwa kuwapa
mafundisho, kutoa ushauri na kuwajenga kiimani.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya na
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Gervas Nyaisonga
amesema kuwa Kanisa linatambua mchango mkubwa wa Serikali na kuunga mkono
mipango ya maendeleo katika utoaji huduma za maji, umeme, barabara, afya na
maeneo mengine.
“Kanisa linatoa pongezi kwa Serikali kwa utekelezaji wa
programu mbalimbali za kumpunguzia mwananchi changamoto za kiuchumi na jamii”.
Kadhalika Askofu Mkuu Nyaisonga ameipongeza Serikali kwa kupinga vitendo vya ushoga na usagaji “endeleeni msimamo huo, kanisa lina msimamo imara wa kupinga vitendo hivyo”.
Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam (wa tatu kushoto) akiongoza Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Mbeya, Godfrey Jackson Mwasekaga na Jubilei ya miaka 125 ya uinjilishaji Jimbo Kuu la Mbeya iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mei 26, 2024. Kushoto ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Gervas Nyaisonga. Waziri Mkuu alimwakilisha Rais Dkt. Samia suluhu Hassan katika ibada hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza Askofu Msaidizi wa jimbo Kuu la Mbeya, Godfrey Jackson Mwasekaga katika ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu huyo na Jubilei ya miaka 125 ya uinjilishaji Jimbo Kuu la Mbeya iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mei 26, 2024. Waziri Mkuu alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassanb katika ibada hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa , Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson na Mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homera (kulia) wakishiriki Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Mbeya, Godfrey Jackson Mwasekaga na Jubilei ya miaka 125 ya uinjilishaji Jimbo Kuu la Mbeya iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mei 26, 2024. Waziri Mkuu alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
0 Maoni