WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali
imejipanga kuendelea kurejesha miundombinu yote ya barabara zilizoathiriwa na
mvua zilizonyesha nchini.
Amesema hayo jana alipokagua daraja lililopo katika kijiji
cha Nambilanje ambalo limeharibika kutokana na mafuriko. Daraja hilo
linaunganisha Wilaya za Liwale na Ruangwa.
“Kwa wakati huu ambao barabara nyingi zimekatika na
kuharibiwa na mvua, Sio mkoa wa Lindi pekee, eneo hili TANROADS wameshafika,
wameangalia hii hali na Waziri wa Ujenzi ameshatoa taarifa kwamba wanaendelea
na uhakiki.”
Amesema kuwa Serikali inasubiri taarifa ya Mamlaka ya Hali
ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kuisha kwa mvua ili itoe fedha na kutangaza
zabuni za ujenzi za ukarabati na matengenezo ya maeneo yote yaliyoathiriwa.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan anatoa pole kwa watanzania wote waliopata athari ya mvua hizo “Nawasihi
muendelee kuwa watulivu na mjenge imani na Serikali yenu Mheshimiwa Rais katika
mipango yake nina uhakika daraja litafanya kazi.”
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amegawa pampu ishirini na
mabomba yatakayotumika kumwagilia kwenye bustani za mbogamboga kwa wakazi
wanaojishughulisha na kilimo hicho eneo la Nandagala wilaya ya Ruangwa mkoani
Lindi.
Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi wachangamkie fursa ya
kilimo hicho kwani kilimo cha mbogamboga kinawezesha mkulima kupata kipato cha
haraka “Tunataka eneo hili liwe kituo kikuu cha upatikanaji wa mazao ya
mbogamboga.”
Aidha, amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mikakati endelevu ya kukuza sekta ya kilimo ikiwemo mpango wa kutumia mabonde mbalimbali nchini ikiwemo yaliyo katika wilaya ya Ruangwa kukusanya maji ya mvua na kuyatumia katika kilimo na mifugo.
0 Maoni