Prof. Muhongo azidi kufanikisha ujenzi wa maabara za Sekondari

 

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, ameanzisha kampeni kabambe ya ujenzi wa maabara tatu za masomo ya Sayansi kwenye kila Sekondari iliyopo jimboni mwake, zikiwemo zile za binafsi.

Ujenzi huo wa maabara zitakazosaidia kuwajengea uwezo wanafunzi wanaosoma masomo ya  Sayansi unachangiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, Mfuko wa Jimbo, Mbunge wa Jimbo, Wanavijiji na Viongozi wao wakiwemo Madiwani.

Kampeni hiyo imepata mafanikio ya kujenga maabara tatu za masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia ni saba kwenye sekondari 7, ambazo ni za Bugwema, Bwai, Ekwabi (Wanyere), Ifulifu, Kiriba, Mugango na Nyakatende.

Taarifa ya Ofisi ya Mbunge Jimbo la Musoma Vijijini, imeeleza kuwa, pia Sekondari zenye maabara mbili na zinakamilisha maabara ya tatu ni tano ambapo ni za Bulinga, Etaro, Makojo, Rusoli na Suguti.

Sekondari kumi na 16 zilizosalia zina maabara moja hadi mbili na zinaendelea na ujenzi wa maabara zilizokosekana, wakati Sekondari tatu ambazo hazina maabara hata moja, nazo hizi zimeanza ujenzi wa maabara tatu.

Prof. Muhongo ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha kampeni hiyo amewaomba wazaliwa wa Musoma Vijijini na Wadau wengine wa Maendeleo kuchangia ujenzi wa Maabara za Masomo ya Sayansi kwenye sekondari za jimbo hilo.

Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini imewaomba wenye nia ya kuchangia kuwasiliana na Viongozi wa Vijijini kwao, wakishindwa wawasiliane na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Musoma au Ofisi ya Mkurugenzi (Musoma DC).

Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21, hadi sasa lina jumla ya Sekondari 28. Kati ya hizo, 26 ni za Kata/Serikali na 2 ni za Binafsi (Madhehebu ya Dini). Kwa sasa jimbo hilo  linajenga Sekondari mpya kumi (10).

Chapisha Maoni

0 Maoni