Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Namibia atembelea Makao Makuu ya Jeshi Dar

 

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Namibia, Air Marshal  Martin Kambulu Pinehas na ujumbe wake  amefanya ziara ya kikazi nchini kwa kutembelea Makao Makuu ya Jeshi Jijini Dar es Salaam na kukutana na mwenyeji wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda.

Air Marshal Penehas alipokelewa na kukagua gwaride rasmi la heshima lililoandaliwa kutoa heshima ya Mkuu wa Majeshi katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, Mkuu wa Majeshi ya ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda alisema JWTZ linafurahishwa kuimarika kwa mahusiano ya diplomasia ya kijeshi yaliyopo kati ya Namibia na Tanzania.

Aidha, amesema kuwa ziara ya Mkuu wa Majeshi wa Namibia itaongeza chachu ya ushirikiano kati ya Majeshi ya nchi hizi mbili hasa katika Nyanja ya mafunzo ambapo majeshi haya yamekuwa yakishirikiana katika mafunzo.

Mkuu wa Majeshi wa Namibia amesema amekuja Tanzania ili kujifunza kutokana na JWTZ kuwa mfano wa kuigwa katika ulinzi.

Chapisha Maoni

0 Maoni