Wanafunzi wa masomo ya Sayansi kunufaika na Samia Scholarship

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imeanzisha udhamini (Scholarship) maalum kwa wanafunzi wanaofaulu masomo ya Sayansi ambapo watasomeshwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa gharama zote zikiwemo za kujikimu, chakula, mabweni na vifaa vya elimu hadi mwanafunzi atakapomaliza masomo yake.

Prof. Mkenda amesema hayo jijini Tanga katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya  ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayozikutanisha taasisi, mashirika, wadau wa maendeleo, asasi, watunga sera, wabunifu/wagunduzi  na wadau wengine kutoka ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya mijadala na kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya elimu, ujuzi na ubunifu.

“Kama wewe ni mwanafunzi unasoma masomo ya sayansi ukafaulu kidato cha sita kati ya wanafunzi bora 640 hadi 700 hapa nchini ukaamua kusoma vyuo vya ndani Tanzania kwenye nyanja za Sayansi, Uhandisi, Elimu Tiba, TEHAMA au Hisabati, wanafunzi hao watasomeshwa kwa asilimia 100 na Serikali, sio mikopo Serikali itakulipia gharama zote na hii inaitwa ‘Samia Scholarship,” amesema Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa maadhimisho  hayo ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yatafanyika mkoani Tanga kwa miaka mitatu mfululizo ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali  katika kuongeza hamasa ya kukuza elimu, ujuzi, na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kusaidia kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii pamoja na kuchagiza maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Chapisha Maoni

0 Maoni