Bilioni 45 zatengwa kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu

 

Waziri wa  Maliasili  na  Utalii  Mhe. Angellah Kairuki (Mb) wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo  kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Bungeni Dodoma, amesema  Serikali itaendelea  kutatua changamoto ya migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu  kwa kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa mwaka 2020 - 2024.

Mhe. Kairuki amesema  shilingi bilioni 45.14 zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya kutatua changamoto  ya  wanyamapori wakali na  waharibifu ikihusisha ununuzi wa helikopta mbili, uchimbaji wa mabwawa 30 katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba, na ujenzi wa vizimba 50 katika maeneo yenye changamoto kubwa ya mamba na viboko katika Halmashauri za Wilaya 18.

Pia, Wizara imepanga kununua ndege zisizo na rubani (drones) 16 na mikanda maalum ya mawasiliano (GPS Satellite Collars)100 kwa ajili ya ufuatiliaji wa mienendo ya wanyamapori katika maeneo ya Kusini, Kaskazini, na Kanda ya Ziwa pamoja na ununuzi wa vifaa vya kudhibiti tembo yakiwemo mabomu baridi elfu 35.

Awali, akieleza namna Wizara inavyotatua changamoto ya migongano kati ya binadamu na wanyamapori kwa mwaka wa fedha unaoendelea, Mhe. Kairuki amesema Wizara imejenga mabwawa 32 katika Mapori ya Akiba na Hifadhi za Taifa kupunguza matukio ya wanyamapori hutoka nje ya hifadhi haswa kipindi cha kiangazi kutafuta maji na chakula.

Wizara imeendelea kutumia teknolojia katika kudhibiti changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu ambapo kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Mei 2024, takriban tembo 451 waliondolewa kwenye maeneo ya wananchi katika Wilaya  nne (4) na kurejeshwa hifadhini kwa kutumia teknolojia ya helikopta.

Hadi kufikia mwezi Mei 2024, jumla ya tembo 35 viongozi wa makundi wamefungwa mikanda maalumu ya mawasiliano (GPS Satellite Collars) katika Mifumo nane (8) ya  Ikolojia li kufuatilia mienendo yao.  

Vilevile, Wizara katika jitihada za kuokoa maisha ya watu na mali zao imevuna  jumla ya wanyamapori 113   wakiwemo nyati 18, tembo 23, viboko 28, mamba 21, simba 3, fisi 9, chui 1 na nyani 10.

Chapisha Maoni

0 Maoni