Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe January Makamba ametumia takribani saa moja kuelezea maeneo ambayo
yatajajadiliwa katika warsha ya Mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi
mbalimbali duniani inayofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius
Nyerere mjini Kibaha kuanzia tarehe 21 hadi 24 Aprili 2024.
Waziri Makamba amewataka washiriki wa warsha hiyo ambao ni
Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi, Wakuu wa Utawala balozini, Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa
Wizara hiyo kujadili kwa upana maeneo hayo ili Wizara iweze kufikia
malengo iliyowekewa na Serikali.
Maeneo ambayo ameyataja, Mhe. Waziri ni pamoja na kuboresha
mawasiliano ndani ya Wizara, baina ya Wizara na taasisi nyingine na wadau wake.
Amesema hakuna namna Wizara ambayo majukumu yake ni uratibu ikafikia ufanisi
unaohitajika bila kuwa na mfumo madhubuti wa mawasiliano.
Amesema eneo lingine ni umuhimu wa Wizara kuweka mfumo
madhubuti zaidi wa kufuatilia utekelezaji wa matukio ambayo imekuwa ikiyaratibu
tena kwa ufanisi mkubwa. Matukio hayo ni pamoja na masuala yanayoafikiwa katika
ziara za viongozi, Mikutano, makongamano ambayo yana faida kubwa kwa nchi kama
yatafuatiliwa vyema utekelezaji wake .
Mhe. Waziri aliongeza kuwa kuna umuhimu wa Wizara wa kuweka mfumo
wa kuwaongezea maarifa, weledi na ujuzi maa fisa wake, hususan katika uandishi
na kuzungumza. Amebainisha kuwa nchi yetu inasifika na kutangazika kutokana umahiri
wa wanadiplomasia wake, jambo ambalo limekuwa ni kama urithi wetu, hivyo lazima
jambo hili liendelezwe kwa kuwapatia watumishi ujuzi unaohitajika.
Suala lingine ambalo Mhe. Waziri amelisisitiza ni umuhimu wa
kuwa na mfumo wa kuwajibishana. Amesema mfumo huo utasaidia kuhamasisha
utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika Wizara.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuendelea kulinda heshima na
hadhi ya nchi yetu huko Nje. Alisema kuwa kufanikisha hilo ni pamoja na kuwa na
mazingira bora ya utendaji kazi huko nje ikiwa ni pamoja na kuwa na vitendea
kazi vinavyohitajika.
Alisema Serikali itahakikisha inaboresha mazingira ya kazi
ili nchi iendelee kulinda heshima yake iliyojengwa kwa muda mrefu na viongozi
waliopita.
Mhe. Waziri alihitimisha mazurngumzo yake kwa kuwapongeza Mabalozi kwa kazi nzuri wanayofanya licha ya changamoto wanazokabiliana nazo. Amesema tokea ateuliwe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa muda wa miezi saba sasa amebaini kuna uwezekano wa kufanya mambo makubwa zaidi na ndiyo moja ya sababu ya kuitisha warsha hiyo ambayo ameitaja kuwa ni ya kubainisha changamoto, kuzitafutia ufumbuzi na kuweka mpango wa utekelezaji wenye tija kwa maslahi ya nchi.
0 Maoni