Serikali ya Tanzania
imezihimiza nchi za ukanda wa SADC kushirikiana katika usimamizi wa Misitu ya
Miombo kutokana na umuhimu wake kiuchumi, kijamii na katika uhifadhi mazingira.
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 17,2024 na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Kimataifa
kuhusu usimamizi endelevu wa misitu ya miombo unaofanyika jijini Washington DC nchini Marekani.
“Tushirikiane na kupeana uzoefu, mbinu na teknolojia bora za
usimamizi na uendelezaji wa misitu ya miombo" Mhe Kairuki alisema.
Aidha, Mhe.Kairuki amezitaka nchi hizo kushikamana kwa
pamoja kukabiliana na kasi kubwa ya uharibifu wa misitu unaotokana na shughuli
za kibinadamu kama vile ukataji miti, kilimo, uchomaji moto na utegemezi wa
nishati ya kuni ” Waziri Kairuki amesisitiza.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ametaja jitihada
mbalimbali za Serikali ya Tanzania katika usimamizi na uendelevu wa misitu ya
miombo kama mpango wa kitaifa wa kuhamia
kwenye nishati safi kutoka katika matumizi ya kuni na mkaa ambapo kufikia mwaka
2031 Tanzania iwe imeshahamia kwenye matumizi ya nishati safi.
Pia amesema Tanzania inaendelea kuimarisha viwanda vya mazao
ya nyuki kwa ajili ya kuwezesha wafugaji wa nyuki kupata fedha na hivyo
kupunguza utegemezi kwenye misitu.
Ameomgeza kuwa pia Tanzania inaendelea kuimarisha usimamizi
wa sheria katika misitu na kuhimiza ushiriki wa jamii katika uhifadhi wa misitu
ikiwa ni utekezaji wa Sera ya Taifa ya
Misitu.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mawaziri, Wabunge na Maafisa Waandamizi kutoka nchi za Zimbabwe, Zambia, Namibia, Msumbiji, Malawi, Congo, Botswana, Angola na Tanzania, Umoja wa Afrika na wadau mbalimbali wa uhifadhi.
0 Maoni