Waziri Mkuu Majaliwa akagua athari za maafa Rufiji

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi waliokumbwa na adha ya mafuriko nchini waendelee kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kuratibu utoaji wa misaada kwenye maeneo yaliyoathirika.

Barabara ya Mkongo hadi Utete na ile ya kutoka Mloka Mkongo zote zimeathirika ambapo amesema Serikali inafanya kazi ya kurejesha mawasiliano ili wananchi waweze kupata huduma muhimu.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo jioni (Jumanne, Aprili 16, 2024) wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Chumbi, wilayani Rufiji, mkoani Pwani ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko kwenye eneo hilo. Hadi sasa waathirika 740 wako kambini.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili Ikwiriri, Rufiji akitokea Mlimba, Morogoro aliwaomba wananchi hao waendelee kutulia kwani serikali iko nao na itaendelea kuwahudumia hadi hali yao irejee katika hali ya kawaida.

Amewataka watendaji wa vijiji waendelee kubaini maeneo mapya ya kuishi ambayo yatatumika kuhamisha kaya zilizoathirika.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza TARURA, TANROADS na TAZARA zishirikiane kufanya ukarabati katika maeneo yote yaliyopata athari wakati Serikali inasubiri kumalizika kwa mvua ili iweze kufanya ukarabati mkubwa.

Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jaffo, Naibu Waziri wa Nchi (OWM-SBU), Ummy Nderiananga, Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi na watendaji wengine.

CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu

Chapisha Maoni

0 Maoni