Jopo la Wataalamu kutoka sekta ya utalii nchini Morocco na
jopo la wataalamu wa Sekta ya Maliasili na Utalii nchini wamekutana na kufanya
mazungumzo yaliolenga kuimarisha ushirikiano katika kutoa huduma bora za utalii
pamoja na kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na Morocco.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho mapema hivi leo,
Naibu Balozi wa Morrocco nchini Lahoucine Rahmouni alisema ujumbe wa wataalamu
watatu kutoka Morocco uliwasili nchini aprili 28, 2024 tayari kujadili kuhusu
namna bora ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania nchi yake
katika sekta ya utalii.
Balozi Rahmouni anasema ujumbe huo unajumuisha Mkuu wa Idara
ya Ushirikiano katika Wizara ya Utalii, Utamaduni, Uchumi wa Jamii na
Ushirikiano, Omar Dinia, Mkuu wa Idara ya Sheria na Ubora katika Wizara ya
Utalii, Utamaduni, Uchumi wa Jamii na Ushirikiano, Zineb Saidi na Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Kitaifa ya Utalii ya Morocco, Sarah Benabdellah.
“Nimepokea jopo la wataalamu kutoka Morocco watakaokuwa
nchini hadi Mei 3, 2024 wakihakikisha wanafanya majadiliano ya kina na
wataalamu wa Sekta ya Utalii nchini ili kuona namna gani nchi hizi mbili
zinaweza kushirikiana katika eneo ya mafunzo ya watoa huduma za utalii, eneo la
uhusiano kwa umma na utangazaji ili pande zote zinufaike,” anasema.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii ya Tanzania (TTB), Ephraim
Balozi Mafuru anasema ujio wa wajumbe hao unafungua fursa mpya ya kuvitangaza
vivutio vilivyopo nchini na kuboresha huduma za utalii ili wageni wa ndani na
nje ya nchi waweze kuvifikia vivutio hivyo.
"Rais Samia Suluhu Hassan ametuheshimisha kama nchi
kupitia Filamu maarufu ya Royal tour, watalii wanamiminika nchini sasa ni muda
muafaka wa kufikiria nini tunafanya kuendeleza jitihada za mama, mkutano huu ni
moja ya mikakati ya nchi kuhakikisha sekta ya utalii na uwekezaji unakuwa
nchini, tutaitumia ipasavyo,” anasema.
Ujio wa wataalamu hao toka Morocco ni matokeo ya mkutano
uliofanyika Rabat, Morocco, kati ya Mhe. January Makamba, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano
wa Kiafrika na Wamorocco wanaoishi Nje, Mhe. Naser Bourita katika siku za
karibuni.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Chuo cha Utalii Tanzania (NCT) Makumbusho ya Taifa ( NMT) pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
0 Maoni