Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Angela Nyaki, Mkuu
wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro amewaaga
vijana wa kitanzania almaarufu Ramadhani Brother’s jana tarehe
29.04.2024 kuianza safari ya ndoto yao ya kuelekea katika kilele kirefu kuliko
vyote Barani Afrika cha Mlima Kilimanjaro chenye urefu wa mita 5,895 kutoka
usawa wa bahari, safari inayotarajiwa kuchukua takribani siku 5 kupitia lango
la Marangu.
Akiwaaga vijana hao waliojizolea umaarufu duniani kutokana
na sanaa yao ya Sarakasi, Kamishna Nyaki alisema, "Lengo la Ramadhan
Brother's kupanda mlima huu kwanza ni kuufahamu vizuri ili wanapouelezea
kimataifa wasiwe na chembe ya mashaka, lakini pia kutangaza vivutio vingine vya
utalii vinavyopatikana Tanzania watakavyotembelea baada ya kushuka mlima huu."
Pamoja na hayo Ramadhani Brother’s wamejikita katika kuhamasisha kampeni maalumu ijulikanayo kama “Vote Now” mahususi kwa ajili ya kupigia Kura Mlima Kilimanjaro na Serengeti zinazowania tuzo za World Travel Awards.
0 Maoni