WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia
ameridhia kutoa tani 189 za mbegu za mpunga, mahindi na alizeti ili zisambazwe
kwa wakulima wa wilaya ya Kilombero.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa pole kwa wananchi wote
walioathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazonyesha nchini, lakini pia
ametoa mbegu hizo ili kuhakikisha wale waliopata athari katika mashamba yao
waweze kuendelea na shughuli za kilimo pale hali itakapokaa sawa,” amesema.
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 16, 2024) wakati
akizungumza na wananchi wa maeneo ya Mlimba, Taweta, Masagati wilayani
Kilombero, mkoani Morogoro ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko.
Waziri Mkuu ambaye pia alikagua bonde la mto Kilombero
linalojumuisha wilaya tatu za Kilombero, Ulanga na Malinyi, amesema Rais Samia
ameelekeza Serikali iendelee kuwahudumia wananchi wote waliopata athari ikiwemo
kuimarisha maeneo ya utoaji huduma za afya, kugawa vyakula na kurejesha
miundombinu ikiwemo barabara na reli.
“Watanzania tuwe watulivu, Serikali yenu ipo kazini. Rais
wetu Dkt. Samia ametupa maelekezo ya kuhakikisha tunawahudumia na kurejesha
hali, tutaleta vyakula na tayari madaktari takribani 20 wameshasambazwa kwenye
mikoa ya Morogoro na Pwani ili waweke kambi za utoaji huduma za afya.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza TARURA,
TANROADS na TAZARA zishirikiane kufanya ukarabati katika maeneo yote yaliyopata
athari wakati Serikali inasubiri kumalizika kwa mvua ili iweze kufanya
ukarabati mkubwa.
Waziri Mkuu anaelekea Ikwiriri, Muhoro na Chumbi wilayani
Rufiji, mkoani Pwani ambako atakagua athari za mafuriko na kuwasalimia
wananchi.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni