Filamu ya The Royal Tour yapaisha idadi ya watalii nchini

 

Filamu ya “The Royal Tour” ambayo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ameshiriki akiwa mshiriki/mwongozaji mkuu imekua na mafanikio makubwa sana katika kutangaza vivutio vya utalii na urithi wa sanaa na utamaduni wa nchi yetu, kwani kupitia filamu hiyo kumekua na ongezeko kubwa la idadi ya watalii nchini ikilinganishwa na kipindi kabla ya kuzinduliwa kwa filamu hiyo.

Haya yamebainika Bungeni wakati Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) akijibu swali la Mhe. Amina Daud Hassan (Mb) ambaye alitaka kujua idadi ya watalii waliongia  nchini tangu kufanyika kwa filamu ya  Royal Tour iliyoasisiwa na Mheshimiwa Rais ili kutangaza nchi yetu.

Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa tangu filamu hiyo izinduliwe idadi ya watalii imeongezeka ambapo kuanzia mwezi Mei hadi Disemba Mwaka 2022 kumekuwa na ongezeko la asilimia 40.38 la idadi ya watalii ambayo ilifikia 1,086,143 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa Mwaka 2021 ambapo idadi ya watalii ilikuwa 647,595.

Aidha, idadi ya watalii iliendelea kuongezeka kwa asilimia 16.6 hadi kufikia watalii 1,302,271 kutoka watalii 1,086,143 kwa kipindi cha Mei hadi Disemba 2023. Vilevile, kwa kipindi cha Januari hadi Disemba Mwaka 2023 idadi ya watalii pia imeendelea kuongezeka hadi kufikia watalii 1,808,205 ukilinganisha na watalii 1,454,920 waliotembelea nchi yetu kwa kipindi kama hicho Mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 24.3.

“Hivyo, ni dhahiri kuwa filamu ya Tanzania “the Royal Tour” imekuwa na matokeo mazuri sana katika sekta ya utalii na ni vema Watanzania wote kwa pamoja tukaunga mkono juhudi za Mhe. Rais” alisema Mhe. Kitandula.

Kwa upande Mwingine Mhe. Kitandula akijibu swali la Mhe. Kilumbe Shaban Ng’enda (Mb) aliyetaka kujua  Serikali ina mpango gani wa kuweka vivutio vya utalii katika mji wa Ujiji ili watu mbalimbali duniani  waweze kutembelea.

Mhe. Kitandula alisema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau katika sekta imeanza  kufanya tathmini ya kina ya njia ya biashara ya watumwa na meno ya Tembo kuanzia katika Mji wa Bagamoyo, Pwani mpaka Mji wa Ujiji, Kigoma kwa lengo la kuibua fursa za utalii na kuboresha vivutio vyote vilivyopo katika njia hiyo; na hivyo kuvutia wageni na watalii kutoka ndani na nje ya Nchi kutembelea maeneo hayo kwa ajili ya kuona kumbukumbu hiyo muhimu Duniani.

Mhe. Kitandula amesema kuwa katika hatua nyingine ya kuboresha vivutio vya utalii wa kihistoria na malikale Nchini, Wizara, imelenga kufanya tathmini ya maeneo yote ya malikale katika Mji wa Ujiji na maeneo mengine nchini ili kutambua umuhimu wake kwa lengo la kuyatunza kulingana na kanuni na sheria husika ili kuhakikisha kuwa uendeshaji wa shughuli za utalii katika maeneo yenye historia na malikale unafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Na Anangisye Mwateba-Bungeni Dodoma

Chapisha Maoni

0 Maoni