Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar
zinafanya jitihada kubwa kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuhimiza
uwajibikaji ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 pamoja na mipango mingine
ya maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi amesema hayo alipofungua rasmi Mkutano wa
mafunzo kwa wajumbe na wataalam wa kamati ya SADCOPAC katika kupambana na
rushwa , kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa maliasili
unaofanyika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, uwanja wa ndege Zanzibar tarehe:
17 Aprili 2024.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar inasimamia
masharti na maelekezo ya miongozo ya kamati ya SADCOPAC kwa kuwa mstari wa
mbele kuhakikisha inatekeleza kikamilifu makubaliano yaliyoafikiwa baina ya
nchi wanachama.
Rais Dk. Mwinyi
amesema Zanzibar imeanzisha utaratibu wa kusomwa hadharani taarifa ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kujadiliwa kwa uwazi na kina katika Baraza la Wawakilishi.
Kwa upande mwingine Rais Dk. Mwinyi ametoa wito kwa nchi wanachama wa SADC kuziimarisha taasisi zinazohusika na utawala bora kwa kuzipatia wataalam zaidi wa fani mbalimbali ili ziwe na upeo mkubwa zaidi wa kufanya uchunguzi kwa mujibu wa majukumu yao.
0 Maoni