CCM yachangia Tsh milioni 10 kwa wananchi waliopatwa na maafa Itezi

 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amewatembelea wananchi waliopatwa na maafa ya kuharibikiwa kwa nyumba na mali zao mara baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini na kusababisha maporomoko ya matope kutoka kwenye Mlima Kawetere, Kata ya Itezi, jijini Mbeya.

Mara baada ya kufika kwenye kambi wanaoishi kwa muda katika Shule ya Msingi ya Tambukareli , Baloz Nchimbi ametanguliza salamu za pole za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan , na kuwapatia kiasi cha Tsh Milioni 10 waathirika  hao ili kupunguza madhila yanayowakabili.

Balozi Nchimbi alikabidhi fedha hizo kusudi kwa mwanamama mmoja kati ya waliopatwa na maafa hayo pamoja na Diwani wa kata hiyo ya Itezi, Sambweshi Tambala ambaye pia amepatwa na maafa.

Akizungumza na wananchi hao, Balozi Nchimbi amesema lengo la kufika hapo ni kuwapa pole na kuwaomba kuendelea kumtanguliza na kumshukuru Mungu kwa kuwanusuru na maromoko hayo.

"Tumshukuru Mungu wote mpo salama, tujaribu kufikiria maporomoko haya yangetokea saa 8 usiku leo tungekuwa tunazungumza nini ? Tumtangulize Mungu sana. CCM inatoa shukrani kwa watu wote walioguswa na kuja kusaidia kambi hili, shukrani pia kwa Serikali, taasisimbalimbali na mbunge wenu, Dk Tulia Ackson .Niwaombe sana ndugu zangu, zingatieni tahadhari za serikali wakati uchunguzi unaendelea, wananchi tuwe na subira tusiharakie kurudi huko, "anasema Balozi Nchimbi

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mjini. Beno Malisa, amemueleza Katibu Mkuu kuwa maporomoko ya matope kutoka mlimani yalitokea Jumapili ya tarehe 14 Aprili, 2024 na kusababisha uharibifu wa nyumba 21 na mali.

 Mafuriko hayo yamesababisha kaya zaidi ya 50 kukosa makazi hali iliyoilazimu Serikali kuwapa makazi ya muda kkatika Shule ya Msingi ya Tambukareli.

 Malisa ameendelea kusema kuwa wananchi hao wamepewa misaada ya huduma za kibanadamu kutoka serikali ya Mkoa Mbeya na wadau mbalimbali.

Vilevile , Malisa amesema wananchi hao wamekuwa wakipatiwa huduma za afya na msaada wa kisaikolojia.

Chapisha Maoni

0 Maoni