Katika mwaka 2024/25, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imepanga
kutumia shilingi bilioni 841.19 kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na ukarabati
wa miundombinu ya barabara za wilaya.
Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 257.03 ni za Mfuko wa
Barabara, shilingi bilioni 127.50 Mfuko Mkuu wa Serikali, shilingi bilioni
325.77 ni za tozo ya mafuta (shilingi 100 kwa lita), shilingi bilioni 4.03 za
mapato ya ndani kupitia Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam na
shilingi bilioni 126.85 ni fedha za nje.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI Mhe. Mohamed
Mchengerwa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Alisema fedha hizo zitaenda kutekeleza matengenezo na
ukarabati wa barabara za wilaya zenye urefu wa Km 20,745.31, ujenzi wa barabara
za lami zenye urefu wa Km 434.50 pamoja na ujenzi wa barabara za changarawe
zenye urefu wa Km 13,802.34.
Aidha, ujenzi wa madaraja 160 na ukarabati wa madaraja 21, ujenzi
na matengenezo ya boksi kalavati 586 na vivuko (drifti) 15, ujenzi wa mifereji
ya maji ya mvua yenye urefu wa mita 141,070.54, ujenzi wa kingo za Mto
Msimbazi, kudhibiti maeneo ya juu ya Mto Msimbazi (upstreams) pamoja na
kuhamisha karakana ya mabasi yaendayo haraka kutoka Jangwani kwenda eneo la
Ubungo Maziwa.
Waziri Mchengerwa aliongeza fedha hizo zitaenda kuboresha
miundombinu shindanishi katika Miji Tanzania (TACTIC) kwa kujenga miundombinu
katika Halmashauri 12 za Majiji ya Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya, Halmashauri
za Manispaa ya Kigoma, Songea, Ilemela, Kahama, Morogoro, Sumbawanga na Tabora
na Halmashauri ya Mji Geita.
Pia miundombinu msingi inajumuisha ujenzi wa masoko, mitaro
ya maji ya mvua, stendi za mabasi, maghala ya kuhifadhia mazao na kujenga
barabara kiwango cha lami Km 147.5, kuondoa vikwazo vya upitikaji barabarani
kwenye wilaya 131 na ujenzi wa barabara kiwango cha lami Awamu ya Pili Km 164
kupitia Programu ya Kuongeza Fursa za Kiuchumi na Kijamii Nchini (RISE) pamoja
na ujenzi wa barabara zenye urefu wa Km 250, kupitia Mradi wa Uendelezaji wa
Jiji la Dar es Salaam Awamu ya 2 ambapo kati ya hizo Km 132 zimefanyiwa
usanifu.
Kwa upande wa matumizi ya teknolojia mbadala kwenye ujenzi wa miundombinu, Waziri huyo alisema kwa Mwaka 2024/25 Ofisi ya Rais- TAMISEMI kupitia TARURA imepanga kuendelea na majaribio ya matumizi ya teknolojia mbadala kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Mikoa ya Pwani, Iringa, Dodoma na Simiyu ambapo jumla ya Km 54.15 zitajengwa kwa kutumia teknolojia ya "Ecoroads".
Na. Catherine Sungura-Dodoma
0 Maoni