Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini
zimeleta athari katika jimbo la Kavuu lililopo katika halmashauri ya Mpimbwe
wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Mvua hizo zilizonyesha usiku wa kuamkia tarehe 14 April 2024
zimekata mawasiliano katika madaraja ya Mto Msadya pamoja na daraja la Mto Kibaoni
katika halmashauri ya Mpimbwe.
Katika eneo la Mto Msadya uliohama njia yake hadi maeneo ya
makazi ya watu na kusababisha adha kwa magari na wananchi wanaotumia daraja
hilo hususan katika vitongoji vya Ikuba, Usenga na Igongo.
Upande wa daraja la kibaoni, mawasiliano baina ya Kibaoni na
Usevya katika halmashauri hiyo ya Mpimbwe yamekatika na kusababisha njia
kufungwa kutokana na maji kuvunja daraja hilo.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendekeo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akiwa na viongozi wa serikali na Chama
cha Mapinduzi wilaya ya Mlele walifika maeneo yaliyoathirika kwa lengo la
kujionea uharibifu na athari iliyopapatikana kwa wananchi.
Mhe. Pinda aliwapa pole wote walioathirika na mafuriko hayo
huku akiwataka wananchi hususan vijana wanaoishi eneo la mto Msadya kuanza
kuchukua hatua za uhifadhi maingira.
"Kipande chote mpaka wa Ikuba na Kashishi lazima
tuungane tuutunze huu mto, kwa hiyo vijana mradi namba moja hapa Ikuba ni mto,"
amesema Mhe. Pinda.
Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi Alhaji Majid Mwanga
alitaka pawepo tahadhari kwenye maeneo yote yaliyoathirika huku akiwataka watendaji
wa kijiji na kata kuzunguka na kupata taarifa ya maeneo yaliyoathirika kwa
kushirikiana na ofisi ya halmashauri ya Mpimbwe ili wilaya ichukue hatua
stahiki.
"Ni imani yangu mkurugenzi utaitisha kikao cha kamati
ya maafa kukaa na kujadili kuona namna
matukio haya yalivyotokea maana siyo hapa tu ili kama wilaya tuweze kutoa
maamuzi na taarifa sahihi," alisema Alhaji Mwanga.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mpimbwe Bi Shamim Daud
Mwariko kwa upande wake amewataka wananchi wanaoishi maeneo yaliyoathirika
kutopita katika njia zisizoruhusiwa kwa kuwa ni vigumu kufahamu muda gani maji
yatajaa.
Amesema, halmashauri yake itafanya tathmini maeneo yote
yaliyoathirika na kuona namna ya kushirikiana na kupunguza changamoto
iliyojitokeza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele Silas Ilumba amewatahadharisha wananchi kutolala katika nyumba zote zilizoloana kutokana na athari hizo za mvua kwa kuwa maji yakishakauka zinaweza kudondoka usiku.
Na. Munir Shemweta- Mlele
0 Maoni