Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
imesema kuwa ina lengo la kuboresha maisha ya wananchi wa tarafa hiyo kwa
kuwaelimisha na kuwahamisha wananchi waliojiandikisha kuhama kwa hiyari kwenda
Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga na maeneo mengine nchini.
Akizungumza na wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kwa nyakati
tofauti katika zoezi la uelimishaji, uhamaishaji na uandikishaji kaimu meneja
wa Uhusiano kwa Umma wa mamlaka hiyo Bw. Hamis Dambaya amesema zoezi la
kuwaelimisha wananchi hao litaendelea ili kuhakikisha kila mkazi wa tarafa ya
Ngorongoro anahama kwa hiyari.
Amewaeleza wananchi hao kwamba serikali haina nia mbaya kwa
kuwashawishi kuhama kutoka ndani ya hifadhi kwani inatambua kuwa iwapo wananchi
hao watakubali kuhama wataweza kuboresha maisha yao katika maeneo mbalimbali
watakayoamua kuelekea sambamba na kulinda usalama wao kutokana na uwepo wa
matukio ya wanyama wakali ndani ya hifadhi.
“Mnaishi katika mazingira magumu hasa kutokana na kukosa
uhuru wa kuingia na kutoka ndani ya hifadhi, kuhofia Wanyama wakali ambao
wamekuwa hatari kwa mifugo na baadhi ya wananchi, serikali imefanya uamuzi
sahihi wa kuwahamasisha ili kuwa na Maisha bora na huru nje ya hifadhi,” alisema
Bw. Dambaya.
Bw. Dambaya amesisitiza kuwa serikali imejipanga vizuri
katika kuhakikisha kila mwananchi anayekubali kuhama kwa hiyari kutoka ndani ya
hifadhi anapata stahiki zake zote za kisheria ikiwemo kitita cha shilingi
milioni kumi wanaohamia msomera na shilingi Milioni kumi na tano wanaohamia
maeneo mengine ambapo fedha hizi zinatolewa kama motisha na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amewataka wananchi hao kuachana na propaganda za baadhi ya
wanasiasa na wanaharakati wasiowatakia mema kwa kuwashawishi kuendelea kubaki
ndani ya hifadhi huku wao na familia zao wakiishi katika miji mbalimbali nchini
na kufanya shughuli zao katika mazingira magumu.
“Msihadaike na watu wenye nia ovu wanaowashawishi mbaki
ndani ya hifadhi, hameni kwa hiyari kuelekea katika Kijiji cha Msomera na maeneo
mengine ambayo huduma za kijamii zimeboreshwa kwa mustakabali wenu na vizazi
vyenu,”alisema Bw. Dambaya.
Katika ziara hiyo ya tarafa ya Ngorongoro timu ya uhamasishaji imeweza kutembelea kaya mbalimbali katika Kijiji cha Naiyobi, Kapenjiro na endulen ambapo wananchi kadhaa walielimishwa na kukubali kuhama kwa hiyari na kuamua kujiandikisha.
0 Maoni