Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb)
amesema kuwa mwelekeo wa serikali kwa sasa ni kujikita katika matumizi ya
teknolojia ya kisasa katika uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na misitu ili kuhakikisha
uhifadhi unakuwa endelevu kwa vizazi vya sasa na baadae.
Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo katika kilele cha maadhimisho
ya siku ya wanyamapori duniani yaliyofanyika jana Babati Mkoani Manyara.
“Pamoja na matumizi ya teknolojia kwenye uhifadhi, Serikali
inatekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuongeza ulinzi kwa wanyamapori
ili kupambana na ujangili wa nyara na Kupunguza migongano kati ya wanyamapori
na wananchi na kuhakikisha kuwa wanyama
wanakuwa salama kwenye Hifadhi zetu,” alisema Kairuki.
Aidha, Waziri Kairuki amezitaka taasisi za uhifadhi kuendelea
kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii ili iweze kuwa sehemu ya uhifadhi endelevu na
kupunguza vitendo vya ujangili wa rasilimali za wanyamapori na misitu.
Akiongea katika maadhimisho hayo mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori Dkt. Fortunata Msofe alisema
shughuli za ulinzi wa wanyamapori na misitu ni la kufa na kupona kwa wadau wote
wa uhifadhi ndio maana katika maadhimisho ya nwaka huu wamekuja na kauli ya kuwa
kauli mbiu isemayo “Kuunganisha watu na ulimwengu, kuvumbua matumizi ya
teknolojia ya kisasa kuhusiana na uhifadhi wa wanyamaopori.”
Dkt. Msofe amebainisha kuwa uamuzi wa kutumia teknolojia
katika uhifadhi unalenga kutatua changamoto za migongano ya binadamu na
wanyamapori.
Akiongea kwa niaba ya Kamishina wa Uhifadhi wa Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro. Afisa Uhifadhi Mkuu wa NCAA Dismas Macha amesema NCAA
kwa sasa inatumia njia mbalimbali za kiteknolojia ili kuhakikisha wanyamapori
wanabaki salama kwenye mazingira yao bila kuathiri shughuli za kibinadamu
“Tunatumia njia
mbalimbali kama visikuma mawimbi, mifumo
ya GPS, kamera za kufuatilia mienendo ya
wanyama, ndege zisizo na rubani "drones" na nyinginezo ambazo zinazotumia teknolojia ya kisasa kutuwezesha kuimarisha ulinzi na usalama wa
wanyamapori ndani ya Hifadhi.”
Amebainisha kuwa njia hizo zinasaidia kukusanya taarifa za
Wanyama pale wanapotoka au kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine hasa
wale Wanyama hatarishi wanaotoka hifadhini na kuingia kwenye makazi ya wananchi
wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi” alisema Macha.
Mamlaka ya Hifadhi ya
eneo la Ngorongoro (NCAA) ni miongoni mwa taasisi za Wizara ya Maliasili na
utalii zinazoshiriki maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani 2024 yanayofanyika
kitaifa Wilayani Babati Mkoa wa Manyara.
0 Maoni